` RC MBONI ATOA WITO KWA TISEZA KUTANGAZA FURSA KUU YA KONGANI YA UWEKEZAJI BUZWAGI

RC MBONI ATOA WITO KWA TISEZA KUTANGAZA FURSA KUU YA KONGANI YA UWEKEZAJI BUZWAGI

RC MBONI ATOA WITO KWA TISEZA KUTANGAZA FURSA KUU YA KONGANI YA UWEKEZAJI BUZWAGI

Sabasaba 2025 – Dar es Salaam

Katika mwendelezo wa ziara katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ametoa wito mahsusi kwa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kuweka msisitizo katika kutangaza mradi mkubwa wa Kongani ya Uwekezaji Buzwagi, ambao unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi kwa Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la TISEZA katika viwanja vya Sabasaba, RC. Mboni alieleza kuwa Kongani ya Buzwagi ni fursa adimu ya uwekezaji inayojengwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali ya Mkoa na Kampuni ya Barrick Tanzania, ambayo hapo awali iliendesha mgodi wa dhahabu katika eneo hilo.

“Pamoja na kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya TISEZA katika kutangaza maeneo maalum ya kiuchumi, natumia fursa hii kutoa rai kwenu kuiangazia kwa uzito stahiki Kongani ya Uwekezaji Buzwagi. Mkoa wa Shinyanga una mpango kabambe wa utekelezaji wa mradi huu kwa kushirikiana na Barrick Tanzania, tukilenga kutimiza kwa vitendo dira na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Tanzania yenye uchumi wa viwanda na fursa kwa wote,” alisema Mhe. Mboni.

Aidha, Mhe. Mhita alibainisha kuwa Shinyanga ipo tayari kupokea wawekezaji kwa sasa kutokana na mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Alieleza kuwa Mkoa una rasilimali zote muhimu kwa uwekezaji ikiwemo:

Ardhi kubwa na salama kwa uwekezaji, upatikanaji wa maji na nishati ya umeme wa uhakika, miundombinu ya kisasa ikiwa ni pamoja na barabara, uwanja wa ndege wa Shinyanga na Kahama, na mtandao wa mawasiliano ya uhakika, nguvu kazi ya kutosha na yenye ari.

“Dhamira yangu kama Mkuu wa Mkoa, na dhamira ya Mkoa kwa ujumla, ni kuhakikisha tunawahamasisha na kuwakaribisha wawekezaji kuja Shinyanga na katika Kongani ya Buzwagi ambayo ni mfano wa dira mpya ya kiuchumi, ambapo mazingira rafiki ya uwekezaji yanapatikana kwa urahisi na usalama,” aliongeza.

Mkoa wa Shinyanga unatoa mwito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hii ya kipekee kupitia Kongani ya Uwekezaji Buzwagi — eneo lenye historia, miundombinu, rasilimali na nia thabiti ya maendeleo ya kweli.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464