

Mratibu mradi wa Ulinzi wa Vijana (Syp) kutoka shirika la TMEPiD John Maliyapamba Komba akizungumza kwenye kikao
Na Sumai Salum-Kishapu
Katika juhudi za kuimarisha ushiriki Wanaume katika afya ya uzazi,nafasi za uongozi na kulea jamii zenye usawa wa kijinsia, Shirika la TMEPiD limeandaa na kufanya kikao maalumu kilichowakutanisha wadau muhimu kutoka sekta mbalimbali katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Juni 20,2025.
Kikao hicho kimewaleta pamoja wataalamu wa afya, walimu wa elimu ya malezi na afya, vijana waelimishaji rika, maafisa wa polisi kutoka dawati la jinsia, viongozi wa dini pamoja na wataalamu wengine wa kijamii.
Lengo kuu la kikao hicho ni kuibua na kujadili changamoto na mbinu za kuimarisha ushirikishwaji wa Vijana wakiume na wasichana katika masuala ya afya ya uzazi,kutokomeza ukatili wa kijinsia na kushiriki nafasi za uongozi katika jamii hiyo kupitia mradi wa "Ulinzi wa Vijana(Safe guarding Young People)"unaotekelezwa na TMEPiD katika Halmashauri ya Kishapu na Msalala kwa Mkoani wa Shinyanga.
Takwimu zinaonesha kuwa ushiriki wa wanaume katika masuala ya uzazi una mchango mkubwa katika kupunguza vifo vya mama wajawazito,udumavu wa watoto na umasikini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mwita Mwijarubi amesisitiza umuhimu wa kutumia elimu hiyo kwa maslahi mapana na chombo cha mabadiliko.
"Niwapongeze TMEPiD kuleta mradi huu Kishapu unaotaraji kukamilika mwaka 2026 hivyo vijana wakipata elimu hii itawapa uwezo wa kujiamini katika masuala ya afya ya uzazi kwani watakuwa na mpangilio wa uzazi,ukatili utaondoka na pia washiriki katika nafasi za uongozi nafasi ya uongozi si ya wazee tu" ,ameongeza Mwijarubu.
Akizungumza katika kikao hicho mratibu mradi kutokaTMEPiD amesema mradi huo umelenga hasa kuwajengea uwezo na uelewa vijana wa kike na kiume kuhusu masuala ya elimu ya afya ya uzazi,kutokomeza ukatili pamoja na kushirikishwa katika uongozi wa ngazi tofauti za maamuzi.
“Mradi huu unalenga si tu kuelimisha vijana wa kiume na kike bali kuwawezesha kuwa mabalozi wa mabadiliko ya kijamii kwa vitendo, tunaamini jamii inakuwa imara zaidi pale ambapo wanaume na wanawake wanashirikiana kikamilifu katika masuala ya afya ya uzazi.”Amesema Komba
Katika kikao hicho, washiriki wamekubaliana kuwa ufanisi wa mradi huo unategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa karibu kati ya sekta mbalimbali na serikali huku Polisi dawati la jinsia wakisisitiza umuhimu wa elimu endelevu kwa wanaume kuhusu haki za wanawake na madhara ya ukatili wa kijinsia.
Viongozi wa dini, kwa upande wao, wameonesha utayari wa kutumia mimbari na madhabahu kuhamasisha waumini wao kuhusu ushiriki chanya wa wanaume katika familia na malezi.
Hata hivyo, changamoto kubwa imekuwa ni mitazamo ya kijamii inayoweka jukumu la uzazi kuwa la wanawake pekee, na hivyo kuwaweka wanaume pembeni katika michakato ya maamuzi ya afya ya familia.
Wameongeza kuwa vijana wanahitajika kupewa elimu ya kiroho,uwezesho wa kiuchumi,Kushirikishwa katika vikao vya maendeleo ya Kata na Halmashauri sambamba na kusikilizwa.
Kikao hicho ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya sekta ya afya, elimu, usalama na viongozi wa dini na kijamii katika kuleta mabadiliko endelevu hivyo jamii hiyo ikiendelea na juhudi hizi kwa pamoja kuna matumaini makubwa ya kuwa na familia bora, zenye maelewano, usawa na afya bora ya uzazi kwa wote.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mwita Mwijarubi (kulia) na maafisa kutoka Shirika la TMEPiD wakiwa kwenye kikao kilichowakutanisha wadau muhimu kuibua na kujadili mahitaji ya vijana na matarajio yao kuhusu afya ya uzazi na ujinsia kupitia mradi wa Ulinzi wa Vijana (Syp) unaotekelezwa na shirika la TMEPiD Juno 20,2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Afisa maendeleo ya jamii Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Joseph Swalala akizungumza kwenye kikao kilichowakutanisha wadau muhimu kuibua na kujadili mahitaji ya vijana na matarajio yao kuhusu afya ya uzazi na ujinsia kupitia mradi wa Ulinzi wa Vijana (Syp) unaotekelezwa na Shirika la TMEPiD Juni 20,2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mwita Mwijarubi akizungumza wakati akifungua kikao kilichowakutanisha wadau muhimu kuibua na kujadili mahitaji ya vijana na matarajio yao kuhusu afya ya uzazi na ujinsia kupitia mradi wa Ulinzi wa Vijana (Syp) unaotekelezwa na shirika la TMEPiD Juni 20,2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Afisa maendeleo ya jamii Kishapu Efrem Kilango akizungumza wakati akifunga rasmi kikao kilichowakutanisha wadau muhimu kuibua na kujadili mahitaji ya vijana na matarajio yao kuhusu afya ya uzazi na ujinsia kupitia mradi wa Ulinzi wa Vijana (Syp) unaotekelezwa na shirika la TMEPiD Juni 20,2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
