
Mhandisi Sebastian Pastory Malunde akionesha Fomu baada ya kuchukua Fomu ya Maombi ya Kugombea Nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Itwangi kupitia Chama Chama cha Mapinduzi (CCM) leo Juni 28,2025.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mhandisi Sebastian Pastory Malunde, mzaliwa wa Tinde, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania Ubunge wa Jimbo Jipya la Itwangi, ambalo limekatwa kutoka Jimbo la Solwa.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo leo Juni 28,2025, Eng. Malunde amesema:
"Nimeamua kujitosa kwenye kinyang’anyiro hiki kwa kuwa mimi ni mzawa wa Jimbo la Itwangi na changamoto zilizopo ninazifahamu vizuri."Eng. Malunde ni Msomi mwenye Astashahada ya Juu ya Uhandisi wa Meli na Shahada ya Uzamili katika Uwekezaji na Utunzaji wa Fedha.
Vipaumbele Vya Maendeleo
Katika maelezo yake, Eng. Malunde ameainisha vipaumbele vyake ikiwa atapewa ridhaa ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Itwangi:
👉Kujenga shule nne (4) za sekondari za kidato cha tano na sita katika kata mbalimbali kati ya 14 zilizopo jimboni.
👉Kufufua skimu za umwagiliaji katika kata za Masengwa, Nyida na Nsalala zilizopo kwenye Bonde la Mto Manonga.
👉Kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama katika vitongoji vilivyobaki.
👉Kujenga vituo vya afya kwenye kata ambazo bado hazijapata huduma hiyo muhimu.
👉Kufikisha umeme katika vitongoji ambavyo havijafikiwa.
👉Kuanza mchakato wa kuanzisha Halmashauri mpya ya Wilaya ya Itwangi pamoja na Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kusogeza huduma karibu na wananchi.
"Nikipewa ridhaa, nitahakikisha mchakato wa kuanzisha Halmashauri ya Itwangi unaanza mara moja pamoja na Hospitali yenye hadhi ya wilaya," amesema Eng. Malunde.