` KLINIKI YA TIBA KWA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA KUJENGWA HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA SHINYANGA

KLINIKI YA TIBA KWA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA KUJENGWA HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA SHINYANGA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

KLINIKI ya tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya inatarajiwa kujengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ikiwa ni jitihada za kutoa msaada wa kitabibu kwa waathirika wa dawa hizo na kuwasaidia kurejea katika hali yao ya kawaida ya maisha.
Hayo yamebainishwa leo Juni 19, 2025, katika kikao cha wadau wa huduma za afya kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT) kilichofanyika mkoani Shinyanga, kikao ambacho kiliandaliwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ajili ya kujadili eneo mahsusi litakalojengwa kliniki hiyo.

Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka THPS George Anatory, amesema ujenzi wa kliniki hiyo unatarajiwa kuchukua miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba 2025, kwa ufadhili wa Benki ya CRDB kwa gharama ya Shilingi milioni 134.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa kliniki hiyo ni hatua kubwa ya mabadiliko kwa mkoa wa Shinyanga, hasa kwa watu wanaokabiliwa na changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya, kwani watapata tiba, ushauri nasaha na huduma za kurekebisha tabia.

“Kliniki hii ya MAT itakuwa ya kipekee mkoani Shinyanga, na itatoa huduma muhimu za afya kwa waraibu wa dawa za kulevya,” amesema Anatory.
Naye Daktari wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Erasmus Mndeme, amepongeza uanzishwaji wa kliniki hiyo, kwamba huduma zinaendelea kupanuliwa,huku akitaja dawa ambayo hutumia katika Tiba ya Waraibu wa Dawa za kulevya kuwa ni Medhadone hasa kwa wanaotumia Heroine.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Karidushi Kubingwa,amewapongeza wadau hao kwamba kuanzishwa kwa Kliniki hiyo mkoani Shinyanga itasaidia kupunguza idadi ya watu ambao wameathirika na dawa za kulevya.
Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Shinyanga Luther Mneney,ambaye pia ni Kaimu Menjea wa CDRB Kanda ya Magharibi,ameshukuru kwa wadau hao wa THPS kwa kuwaona na kuamua kushirikiana nao katika kuihudumia jamii.

Amesema ujenzi wa Kliniki hiyo ni sehemu ya Benki hiyo kurudisha faida kwa jamii ambayo huitoa ya asilimia 1, na kwamba Kliniki hiyo inakwenda kugusa watu ambao wanaishi maisha magumu baada ya kuathiriwa na dawa za kulevya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile, akiendesha majadiliano ya wadau kuhusu eneo la ujenzi, alitaja maeneo yaliyopendekezwa kuwa ni Kituo cha Afya Kambarage, Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Hata hivyo, baada ya majadiliano hayo wadau walikubaliana kwa pamoja kuwa kliniki hiyo ijengwe katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Kupitia ujenzi wa kliniki hiyo, idadi ya vituo vya "MAT" nchini itaongezeka, na hivyo kupanua wigo wa utoaji wa huduma kwa watu wanaotumia dawa za kulevya,na kuboresha upatikanaji wa huduma za kuokoa maisha.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka THPS George Anatory akizungumza.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile akizungumza.
Naye Daktari wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk.Erasmus Mndeme akizungumza.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Karidushi Kubingwa akizungumza.
Mhandisi James Niwagila akionyesha mchoro wa ujenzi wa Kliniki ya waraibu wa dawa za kulevya katika Mkoa wa Shinyanga.
Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Shinyanga Luther Mneney akizungumza.
Awali Wadau wakitembelea maeneo ambayo yalipendekezwa kwa ajili ya kujengwa Kliniki ya waraibu wa dawa za kulevya,ili kupendekeza eneo moja tu katika ya Kituo cha Afya Kambarage,Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Kikao kikiendelea cha kujadili wapi itajengwa Kliniki ya tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya mkoani Shinyanga,ambapo eneo pendekezwa wajumbe wameridhia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464