Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali wilaya ya Shinyanga (NGOs)yameilalamikia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),kwa kuwapiga faini kutokana na kuchelewa au kushindwa kuwasilisha “Zero Return” kwa wakati hata pale ambapo hawana mapato.
Hayo yamebainishwa leo Juni 27,2025 na Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCONGO)wilaya ya Shinyanga Lucas Daudi,wakati akisoma Risala kwenye Jukwaa la Mwaka la Mashirika hayo wilayani humo,kwa Mgeni Rasmi Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro.
Amesema,licha ya Mashirika hayo kuwa na mchango mkubwa kwa serikali katika kuhudumia jamii,lakini bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)kuwapiga faini “Zero Return” kutokana na kuchelewa au kushindwa kuwasilisha taarifa zao kwa Mamlaka hiyo,hata pale ambapo hawana mapato kutokana na kukosa fedha za miradi.
“Mapendekezo yetu kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Iandae mfumo rafiki kwa Mashirika yasiyo ya Kiserikali,ikiwa ni pamoja na kuondoa faini kwa Mashirika yasiyo na mapato,sababu ya kukosa fedha za kuendeshea miradi,”amesema Lucas.
Pia,wameomba mafunzo ya mara kwa mara kutoka kwenye Mamlaka hiyo kuhusu taratibu za kifedha.
Ametaja changamoto zingine ni kuwa, Mashirika ambayo yanatekeleza miradi zaidi ya mkoa mmoja hukumbwa na ucheleweshaji au kukataliwa kwa vibali kutoka Wizarani, pamoja na ushushwaji wa taarifa kwenda kwenye wilaya za utekelezaji wa miradi ambapo barua huchelewa sana na kuzuia ufanisi wa kazi zao.
“Mapendelezo yetu Ofisi ya Msajili wa NGOs Iandae mfumo wa kibali kimoja (National Permit) kwa miradi ya kitaifa au ya Mikoa ili kupunguza Urasimu,”amesema Lucas.
Aidha,amemuomba Mkuu huyo wa wilaya kwamba aendelee kuwa bega kwa began a Mashirika hayo,pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto hizo,ili kuimarisha uhusiano mzuri kati ya Serikali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa manufaa ya wananchi wote wa Shinyanga.
Naye Dk.Kulwa Meshack kutoka Shirika la Lifeline, akiwasilisha mada kwenye Jukwaa hilo,amekazia suala la kodi, kwambaulipaji wa kodi ni ngumu sana kwa NGOs, sababu mashirika hayafanyi biashara, bali hujitolea kutoa huduma kwa jamii.
Ameiomba pia Serikali,kwamba fursa za Kitaifa ni vyema zikiwa zinashushwa ngazi za chini na kupewa NGOs kzifanya kazi hizo,na siyo watu kutoka makao makuu,na wakati wao wanaziweza,na kutolea mfano utolewaji wa elimu ya mikopo kwa vijana,ambapo wao wanaweza kuifanya kazi hiyo tena kwa ufanisi mkubwa, na hata kuzuia mikopo hewa.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,amepongeza Mashirika hayo kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kwa jamii na kushirikiana na Serikali,huku akiwasisitiza kuzingatia sheria,pamoja na kupeleka taarifa TRA mapema,kwamba hawana mapato kwa sasa ili kutopigwa faini.
“Ofisini kwangu ni na Barua za NGOs kulalamika TRA wanawadai fedha,wewe unajua kabisa hufanyi kazi na upaswa kufanya nini,”amesema Mtatiro.
Aidha,ametoa wito kwa Mashirika hayo yawe na mipango endelevu, kuwa licha ya kukosa fedha kutoka kwa wafadhili, basi waendelee kusimama na kuendelea na shughuli zao kama kawaida, na kwamba Mashirika mengi yakikosa ufadhiri yana kwama.
Katika hatua nyingine, amewasisitiza kuendelea kuelimisha jamii juu ya kulinda Amani na Utulivu wanchi,hasa kwenye kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu 2025,pamoja na vijana wasitumike vibaya kuvuruga Amani ya Nchi.
Katika Jukwa hilo Mashirika yaliyofanya vizuri katika maeneo mbalimbali yalipewa vyeti vya pongeza,likiwamo Shirika la ICS,PACESHI,WAYDS,THUBUTU AFRICA,OPE,TYC, YAWE,LIFELINE,LIFE WATER,WORD VISSION,AFYA PLUS NA RAFIKI SDO.pamoja na vyeti vya pongeza kwa wawezeshaji ambao ni Gelard Ng’ong’a, Dk.Kulwa Meshack,Charles Deogratius,Revocatus Machumula na John Eddy.
Kauli Mbiu ya Jukwaa hilo inasema”Tathimini ya miaka mitano ya mchango wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa,tukiangazia Mafanikio,Changamoto na Fursa.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mwenyekiti wa NaCONGO wilaya ya Shinyanga Lucas Daudi akizungumza.

Mwezeshaji Gerald Ng'ong'a kutoka Shirika la Rafiki SDO,akiwasilisha Mada ya Utawala Bora na Uwajibikaji wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Mwezeshaji Dk.Kulwa Meshack kutoka Shirika la Lifeline,akwiasilisha Mada ya Uzingatiaji wa Sheria na kanuni na changamoto za Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na Mapendekezo.
Mwezeshaji Charles Deogratius kutoka Shirika la WAYDAS akiwasilisha Mada ya Ushawishi wa Sera na ushirikiano wa kimkakati wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Mwezeshaji Revocatus Machumula akiwasilisha Mada ya Mpango Mkakati,Maendeleo na Uendelevu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Jukwaa likiendelea.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akitoa vyeti vya pongezi kwa Mashirika yaliyofanya vizuri katika maeneoe mbalimbali, pamoja vyeti vya pongeza kwa wawezeshaji wa Jukwaa hilo.
Picha za pamoja zikipigwa.
Pia katika Jukwaa hili,imetolewa elimu ya Hifadhi ya Jamii kutoka NSSF,Elimu ya Maadili kutoka TAKUKURU na Elimu ya Uraia kutoka Uhamiaji.