` MADAKTARI BINGWA 43 WA MAMA SAMIA WATIA KAMBI SHINYANGA

MADAKTARI BINGWA 43 WA MAMA SAMIA WATIA KAMBI SHINYANGA


Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MADAKTARI 43 wanaojulika kama Madaktari Bingwa wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,wamewasilia mkoani Shinyanga, kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mkoa huo.
Madaktari hao wamewasili leo Juni 23,2025 na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, na kisha kusambazwa katika halmashauri zote sita za mkoa huo na watatoa huduma ndani ya siku 6 hadi Juni 28.

Macha akizungumza kwenye mapokezi ya Madaktari hao,amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kujali Afya za wananchi wake,na kwamba licha ya kuboresha huduma za Afya,pia ameendelea kuleta Madaktari Bingwa na kuweka Kambi,kwa kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya imara.
“Natoa wito kwa wananchi wote wa Shinyanga, wajitokeze kwa wingi kwenda kupata huduma za kibingwa kwa Madaktari hawa,ambao wapo katika Halmashauri zote sita,”amesema Macha.

Amewapongeza pia Madaktari hao kwa uzalendo ambao wamekuwa wakiuonyesha,pamoja na kumuunga Mkono Rais Samia katika utoaji wa huduma bora ya Afya kwa wananchi na hata kuwafikia wananchi wa pembezoni.
Aidha,Macha ameelezea mafanikio katika Sekta ya Afya mkoani humo ndani ya miaka minne ya Rais.Dk.Samia kwamba ameshatoa kiasi cha sh.bilioni 77 kwa ajili ya ujenzi wa Majengo,ununuzi wa vifaa tiba pamoja na madawa.

“Mfano mwaka 2021 tulikuwa na hospitali za wilaya mbili,lakini ndani ya miaka minne ya Utawala wa Rais Samia tuna Hospitali za Wilaya Saba,pamoja na kuanza kutoa huduma Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa na ina vifaa tiba vya kutosha na Madaktari Bingwa,”amesema Macha.
Kiongozi wa Madaktari hao kutoka Wizara ya Afya Grace Mariki,amesema kwamba watakuwa mkoani Shinyanga kwa muda wa siku sita, na kwamba wapo madaktari wa Magonjwa ya wanawake, watoto,upasuaji,magonjwa ya ndani,kinywa na meno,ganzi,masikio,pua na koo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile,amesema kwamba ujio huo wa Madaktari Bingwa mkoani humo,utawapatia pia ujuzi wa Kibingwa Watumishi wa Afya katika mkoa huo.

Nao baadhi ya Madaktari hao akiwamo Joackim Kisaka, wamesema wapo tayari kuwa hudumia wananchi wa mkoa huo,na kutoa wito kwao wajitokeze kwa wingi.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza.
Afisa kutoka Wizara ya Afya Grace Mariki akizungumza.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile akizungumza.
Picha ya pamoja.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464