RC MACHA: MAUAJI YA WAZEE SHINYANGA KWA KUKATWA MAPANGA SABABU YA IMANI ZA KISHIRIKINA IMEBAKI KUWA HISTORIA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amesema kwamba kutokana na serikali kuwajali wazee pamoja na kuimarisha ulinzi wa kutosha dhidi yao,sasa hivi mauaji ya wazee kwa kukatwa mapanga yaliyokuwa yakisababishwa na Imani potofu za kishirikina mkoani humo hayapo tena na kubaki kuwa historia.
Macha amebainisha hayo leo Juni 14,2025, wakati akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa Kongamano la siku ya kuelimisha na kupinga ukatili dhidi ya wazee duniani,ambalo kitaifa linafanyika mkoani Shinyanga.
Amesema wazee ni Tunu ya Taifa,hivyo wanapaswa kulindwa kwa gharama yoyote ile dhidi ya vitendo vya ukatili,na kwamba kwa kudhihirisha hilo, serikali imekomesha mauaji ya wazee mkoani Shinyanga yaliyokuwa yakifanyika kwa kukatwa mapanga sababu ya Imani potofu za kishirikina.
“Serikali itaendelea kuwa thamini wazee, kuwatimizia mahitaji yenu,pamoja na kuwalinda,zamani hapa Shinyanga kulikuwa na tatizo la mauaji ya wazee kwa kukatwa mapanga sababu ya Imani potofu za kishirikina,lakini sasa hivi hakuna tena na imabaki kuwa historia,”amesema Macha.
Amesema, serikali pia itaendelea kuboresha huduma za matibabu kwa wazee, pamoja na upatikanaji wa madawa ya magonjwa ya wazee,na kuendelea kutengwa madirisha ya wazee kwenye huduma zote za afya, na uwekwaji wa mabango ya mpishe mzee apate huduma kwanza.
Katika hatua nyingine,amewataka vijana kuwatunza wazee wao,na kuacha tabia ya kuwatelekeza pamoja na kuwaachia wajukuu,huku wakijua kabisa hawana nguvu tena za kufanya kazi.
Naye Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu,amewasisitiza vijana wasiwaone wazee wao kama mzigo,bali ni baraka na hazina kwao,ambapo wanapaswa kuwatumia na kuchota busara zao,na kwamba wazee ni Tunu ya Taifa hivyo wasifanyiwe ukatili.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anne Makinda,amesema wazee kwa nchi nzima wapo Milioni 3.5, na kwamba hiyo ni hazina kubwa kwa Taifa ambayo inapaswa kulindwa.
Mwakilishi wa Help Age Tanzania Joseph Mbasha,amesema Jamii inayothamini wazee ni yenye uhai na maadili,na kusisitiza kwamba wazee walindwe na kutimiziwa mahitaji yao,ikiwamo kuboreshwa kwa sera ya wazee ya 2003,kuongezwa kwa bajeti za wazee pamoja na kulipwa Pesheni Jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa David Sendo,amesema Kongamano hilo liwe ni sehemu ya kuleta mapinduzi na kubadilisha maisha ya wazee, sababu wao licha ya kulipigania taifa hili,lakini wamekuwa wahanga wakubwa wa matukio ya ukatili,kukosa matibabu ya uhakika,vipato,pesheni jamii na sheria ya wazee.
Amesema wanahitaji kutekelezewa mahitaji yao yote,pamoja na kuacha kubaguliwa kwa kunyang’anywa mali kama vile ardhi na kudhurumiwa nyumba,huku wakikipongeza Chama cha Mapinduzi CCM,kwa kuingiza masuala ya wazee kwenye Ilani yao ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030.
Kauli Mbiu ya Kongamano hilo inasema: Wazee ni hazina kwa Taifa,tuwalinde na tuwatunze.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anne Makinda akizungumza.
Mwakilishi wa Help Age Tanzania Joseph Mbasha akizungumza.
Naye Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu akizungumza.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa David Sendo akizungumza.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza.
Kongamano likiendelea.
Picha za pamoja zikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464