Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga na Mwanza katika kijiji cha Sayu kata ya Pandagichiza Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga _ Picha na Kadama Malunde
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga na Mwanza katika kijiji cha Sayu kata ya Pandagichiza Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga

Na Kadama Malunde - Shinyanga
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo Mkoa wa Shinyanga, kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli na yanayogusa maisha yao ya kila siku.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Mei 3, 2025 katika Kijiji cha Sayu, Kata ya Pangagichiza, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, NGerson Msigwa, amesema kuwa serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa katika sekta za afya, elimu, miundombinu na maji.
Msigwa amesema kuwa zaidi ya Shilingi bilioni 10 zimetumika kwenye ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba, pamoja na ukarabati wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga pekee.
Ameeleza kuwa miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Rais Samia kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na makazi yao.
"Serikali imekuwa ikitoa fedha moja kwa moja kwenye halmashauri ili kusogeza huduma kwa wananchi. Tunachokiona hapa Sayu ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya serikali katika kuboresha maisha ya watu," amesema Msigwa.
Aidha, ameeleza kuwa kupitia Programu ya BOOST ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu, shule nyingi zimejengwa na madarasa kuongezwa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Vilevile, katika sekta ya maji, miradi kadhaa imetekelezwa na mingine inaendelea ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.
Msigwa amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo, na kusisitiza kuwa Rais Samia amedhamiria kuleta maendeleo kwa vitendo, sio kwa maneno.
Mkutano huo ni sehemu ya ziara ya Msemaji Mkuu wa Serikali inayolenga kuelimisha wananchi kuhusu kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita na kutoa mrejesho wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi.