IMANI YA USHIRIKINA NA MARADHI MKOANI KAGERA, SERIKALI YAWATAKA WANANCHI WAFIKE HOSPITALI

 



RC Kagera Azindua Rasmi Huduma za Madaktari Bingwa, Awataka Wananchi Kuachana na Imani za Kishirikina

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa, amezindua rasmi huduma za madaktari bingwa mkoani humo na kuwataka wananchi kuachana na imani potofu zinazoelekeza matatizo ya kiafya kwenye uchawi, badala yake wajikite katika kutumia huduma za matibabu zinazotolewa na wataalamu wa afya.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Mei 5, 2025, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Mhe. Mwassa alisema kuwa jumla ya madaktari bingwa 41 wamewasili mkoani humo kwa ajili ya kutoa huduma kwa kipindi cha siku tano, kuanzia Mei 5 hadi Mei 9, 2025.

“Kumekuwepo na mtazamo potofu miongoni mwa jamii kwamba mtu akiugua au kufariki lazima ahusishwe na uchawi. Ni muhimu kuelewa kuwa huduma za kibingwa sasa zipo karibu. Usiamini kuwa umelogwa—njoo hospitali, utibiwe,” alisisitiza Mwassa.

Mkuu huyo wa mkoa alibainisha kuwa serikali inaendelea kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi kwa kuimarisha miundombinu ya afya, kusambaza vifaa tiba vya kisasa na kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu, hasa katika maeneo ya pembezoni mwa nchi. Alieleza kuwa hatua hiyo pia inaunga mkono juhudi za kukuza utalii wa tiba, kwa kuvutia wagonjwa kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dkt. Mseleta Nyakiroto, alisema kuwa zaidi ya wananchi 2,000 walijitokeza kupata huduma katika siku ya kwanza ya uzinduzi, idadi ambayo imevuka lengo la awali la kuhudumia watu 1,500.

“Ujio wa madaktari bingwa si tu unarahisisha upatikanaji wa huduma bora za matibabu, bali pia unatoa fursa ya mafunzo kwa wataalamu wa ndani na kupunguza utegemezi wa rufaa kwenda hospitali za kanda au taifa,” alisema Dkt. Nyakiroto.

Naye Mwenyekiti wa Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Kanda ya Ziwa, Kibwana Mfaume, alieleza kuwa kaulimbiu ya zoezi hilo ni “Madaktari Bingwa wa Samia Tumekufikia Ulipo, Karibu Tukuhudumie.” Aliongeza kuwa kuanzia Mei 12, 2025, madaktari bingwa wataanza kutembelea hospitali za wilaya katika halmashauri zote za mkoa wa Kagera.

Mfaume aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kufaidika na huduma hizo za kitaalamu, akisisitiza kuwa serikali inaendelea kutafuta suluhu za changamoto zinazowakabili wananchi katika kutafuta huduma bora za afya kwa gharama nafuu na kwa wakati.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464