` TAKUKURU YADHIBITI UBADHIRIFU WA MILIONI 92 ZA WAKULIMA WA TUMBAKU USHETU, SHINYANGA

TAKUKURU YADHIBITI UBADHIRIFU WA MILIONI 92 ZA WAKULIMA WA TUMBAKU USHETU, SHINYANGA



Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari

Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kudhibiti ubadhirifu wa kiasi cha shilingi milioni 92.16 zilizotengwa kwa ajili ya kuwafidia wakulima wa tumbaku wa Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) Ibambala, kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mkoani humo.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 27, 2025 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga.

Kwa mujibu wa Kessy, fedha hizo zilitolewa kwa wakulima waliopata hasara kutokana na mafuriko yaliyoathiri uzalishaji wa tumbaku katika msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024, lakini hazikufika kwa walengwa kama ilivyokusudiwa.

“TAKUKURU ilibaini kuwa shilingi milioni 11.62 zilichukuliwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kwa matumizi yao binafsi, akiwemo Katibu Meneja Bw. Charles Alex Shiyengo na Mwenyekiti Bi. Faida Paulo Deda,” amesema Kessy.

Aidha, amesema TAKUKURU imebaini kuwa kiasi kikubwa cha fedha ,shilingi milioni 151.53 kiligawiwa kwa watu wasiostahili, wakiwemo ndugu wa viongozi hao.

"Miongoni mwa waliopokea fedha hizo ni Bi. Lucy Masanja Gidabita, mke wa Katibu Meneja, ambaye alipokea shilingi milioni 34.58, pamoja na Bw. Charles Charles Masanja aliyelipwa shilingi milioni 5.58.

Hatua za awali za kurejesha fedha hizo zimeanza kuchukuliwa huku wahusika wakikabiliwa na hatua za kisheria",ameongeza.

Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025, TAKUKURU Shinyanga pia imepokea jumla ya taarifa 57 za tuhuma za rushwa, ambapo 52 zilifanyiwa uchunguzi na 13 kati yake zimefikishwa mahakamani.

Kwa upande wa elimu kwa umma, amesema taasisi hiyo imeendesha mikutano ya hadhara 61, semina 30, na vipindi vya redio na runinga 13 kupitia programu yao ya Takukuru Rafiki, lengo likiwa ni kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.


Kessy amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa njia ya simu ya bure 113 au kupitia tovuti yao ya www.pccb.go.tz.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464