SERIKALI KUENDELEA KUPUNGUZA VIFO VYA UZAZI:RC MACHA

SERIKALI KUENDELEA KUPUNGUZA VIFO VYA UZAZI:RC MACHA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

SERIKALI imeweka lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuboresha afya ya mama na mtoto.
Hayo yamebainishwa leo Mei 5, 2025, katika maadhimisho ya siku ya mkunga duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amesema serikali chini ya uongozi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuboresha huduma za afya ili kufikia malengo hayo.
“Takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa mwaka 2015/2016 kulikuwa na vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Mwaka 2022 idadi hiyo ilipungua hadi 104, na lengo ni kufikia 70 ifikapo mwaka 2030,” amesema Macha.

Aidha,amewataka wajawazito kupenda kujifungua katika vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo ni salama na vina wataalamu wa kutosha, hatua itakayosaidia kupunguza zaidi vifo vya uzazi.

“Takwimu zinaonyesha wajawazito wanaojifungulia kwenye vituo vya afya wameongezeka, kutoka asilimia 63 mwaka 2016 hadi asilimia 81 mwaka 2025,” ameongeza.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk.Yudas Ndungile, amesema mafanikio hayo yametokana na maboresho makubwa katika sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali mpya nne, vituo vya afya 18, ukarabati wa hospitali kongwe mbili na ongezeko la vituo 86 vya kutolea huduma kwa wajawazito.

Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Saturini Manangwa, amesema zaidi ya asilimia 90 ya huduma za mama na mtoto hutolewa na wakunga, na kuwasihi waendelee kutoa huduma zenye ubora, pamoja na kufuata maadili na kuzingatia viapo vyao.
Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA),Dk. Beatrice Mwilike, amesema wakunga wanachangia kwa asilimia 87 katika kupunguza vifo vya uzazi, na wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya kuboresha huduma hizo.

Ameiomba pia Serikali kuongeza idadi ya Wakunga kwenye huduma za afya, huku akimpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya hapa nchini, na hata kuweka mazingira mazuri ya wakunga katika utoaji wa huduma kwa Wajawazito.
Katika hatua nyingine ameiomba serikali iwe inawashirikisha Wakunga kwenye Kamati za Maafa kama Wajumbe,ili wawe wanaweka mazingira mazuri kwa ajili ya kujifungua Wajawazito.

Maadhimisho ya Siku ya Mkunga Duniani mwaka 2025 yamebebwa na kauli mbiu isemayo: “Mkunga ni Nguzo Muhimu katika Kila Janga.”

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni akizungumza.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Peter Masindi akizungumza.
Rais wa TAMA Beatrice Mwilike akizungumza.







Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464