WAANDISHI WA HABARI WAPATIWA MAFUNZO YA USALAMA NA ULINZI

WAANDISHI WA HABARI WAPATIWA MAFUNZO YA USALAMA NA ULINZI

Na Marco Maduhu,ARUSHA

WAANDISHI wa habari wamepewa mafunzo ya usalama na ulinzi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yametolewa leo Aprili 28,2025 katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yanaendelea jijini Arusha.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-Tanzania), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (OJA-DACT).
Mwenyekiti wa MISA-Tanzania Edwin Soko,amesema mafunzo ya usalama na ulinzi kwa waandishi wa habari ni muhimu sana, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia usalama wao.

"Mafunzo ya usalama na ulinzi kwa waandishi wa habari, ni muhumu sana katika utekelezaji wa majukumu yao ili wapate kuwa salama,"amesema Soko.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo imeendelea kushughulikia madhira yanayowakumba waandishi wa habari kazini, ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wa kisheria, kuwadhamini na kuwawekea Mawakili katika kesi zinazowakabili.

Kwa upande wake Afisa Programu kutoka UTPC Victor Maleko, akiwasilisha ripoti ya hali ya usalama wa waandishi wa habari kwa mwaka 2024, alisema waandishi 26 waliripotiwa kukumbana na madhila kazini, wakiwemo wanaume 22 na wanawake 4. na kubainisha kuwa mikoa ya Mwanza na Dodoma inaongoza kwa matukio hayo.
Naye,Emmanuel Mkojela kutoka Jamii Africa akiwasilisha mada kuhusu usalama wa waandishi, aliwasisitiza waandishi kuwa makini na vifaa vyao vya kazi,akieleza kuwa vifaa hivyo ni sehemu muhimu ya ulinzi wao.

Mwenyekiti Mstaafu wa MISA-Tanzania na Mhariri wa Gazeti la Nipashe, Salome Kitomari, aliipongeza MISA-Tanzania, UTPC na OJA-DACT kwa mshikamano wao katika kusaidia waandishi wa habari wanaopitia changamoto mbalimbali wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Mkurugenzi wa UTPC Kenneth Simbaya, amesoma maazimio yaliyopendekeza wakati wa mjadala kwamba kuwepo kwa ushirikiano mkubwa zaidi kati ya Serikali na wadau wa habari kuhusu masuala ya ulinzi na usalama wa waandishi wa habari, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma kati ya taasisi za habari.

Maadhimisho haya ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yataendelea kesho kwa siku ya pili yakibeba kaulimbiu isemayo,"Athari za Akili Bandia kwa Uhuru wa Vyombo vya Habari na Tasnia ya Habari."

TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa Misa-Tanzania Edwin Soko akizungumza.
Mkurugenzi wa UTPC Kenneth Simbaya akizungumza.
Afisa Programu wa UTPC Victor Maleko akiwasilisha mada.
Emmanuel Mkojela kutoka Jamii Africa akiwasilisha mada.
Mafunzo yakiendelea.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464