SERIKALI KAHAMA KUWACHUKULIA HATUA KALI WATU WATAKAOPOTOSHA CHANJO YA PILI YA POLIO
Na Salvatore Ntandu, KAHAMA
SERIKALI ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, imesema haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu watakaobainika kufanya upotoshaji kuhusu chanjo ya pili ya polio kwa watoto wenye umri wa miezi tisa, inayotarajiwa kutolewa ili kuimarisha kinga ya miili yao.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, wakati wa kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi kilichojumuisha Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu, Kamati ya Usalama, viongozi wa dini, na wazee maarufu kutoka Halmashauri za Msalala, Ushetu, na Manispaa ya Kahama.
Mhita amesema kuna baadhi ya watu wameanza kueneza upotoshaji kwa lengo la kuwazuia wazazi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo kwa maslahi yao binafsi, jambo ambalo serikali haitavumilia.
"Chanjo hii ni salama na haina madhara kwa binadamu. Serikali inalenga kuwalinda watu wake,zoezi la chanjo litaanza rasmi Mei Mosi mwaka huu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya. Naomba wazazi, viongozi wa dini, na wazee maarufu wahamasishe wananchi wawapeleke watoto kupata kinga dhidi ya ugonjwa huu hatari wa polio," amesema Mhita.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yuda Ndungile, amesema chanjo hiyo ya polio ya sindano (IPV2) inalenga kuimarisha kinga kwa watoto kutokana na kuwepo kwa matishio ya ugonjwa huo katika nchi jirani.
"Kwa sasa tunaendelea na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chanjo hii, na Mei Mosi tutaanza rasmi kuwapatia watoto chanjo. Tunasisitiza wazazi wawapeleke watoto wao ili wapate kinga dhidi ya ugonjwa wa polio ambao ni hatari katika makuzi yao," amesema Dkt. Ndungile.
Naye mkazi wa Msalala, Emmanuel Madata, alishuhudia jinsi mwanawe (jina linahifadhiwa) alivyopata ulemavu mwaka 1982 kutokana na ugonjwa wa polio baada ya kukosa elimu sahihi kuhusu ugonjwa huo.
"Polio ni ugonjwa hatari. Mwanangu alipata polio na nilimpeleka kwa mganga wa jadi badala ya hospitali. Matibabu hayakusaidia na hatimaye alibaki na ulemavu wa kudumu, nashukuru Mungu anaendelea vizuri, lakini ulemavu huo ungeweza kuepukika, wazazi, tusifiche watoto wetu, tuwapeleke wakapate chanjo hii muhimu," amesema Madata.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wote watakaohamasisha upotoshaji wa chanjo hiyo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464