WAZIRI MKUU MAJALIWA:SERIKALI IMEANZISHA MCHAKATO WA KUANDAA SERA YA AKILI MNEMBA
Na Marco Maduhu,ARUSHA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,amesema Serikali imeanzisha mchakato wa kuandaa Sera ya Akili Mnemba, ili kuhakikisha teknolojia hiyo inaendana na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari,uwazi na uadilifu katika taaluma ya uandishi wa habari.
Majaliwa amebainisha hayo leo Aprili 29, 2025, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yanayofanyika Jijini Arusha.
Amesema sambamba na mchakato wa kuandaa sera hiyo mpya, Serikali pia inaendelea kupitia upya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003, ili kuhakikisha inaimarisha na kulinda taaluma ya uandishi wa habari nchini.
“Hivyo, kupitia mijadala yenu katika maadhimisho haya,toeni maoni yenu kuhusu namna sera hiyo ya Akili Mnemba inavyopaswa kuwa, ili iendane na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari,” amesama Majaliwa.
Amewasihi pia waandishi wa habari kutumia teknolojia ya Akili Mnemba kama nyenzo ya kuwasaidia kutekeleza majukumu yao, badala ya kuwa kikwazo kwa uhuru wa habari.
“Ukweli ni kwamba teknolojia hii ya Akili Mnemba inaweza kuwa msaada mkubwa katika kuboresha kazi zenu, lakini pia inaweza kuwa chanzo cha changamoto kubwa iwapo haitatumika kwa busara na uangalifu,”amesisitiza.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kulinda uhuru wa habari kwa vitendo kwa kushirikiana na waandishi wa habari, na kwamba tayari wameunda kamati ya kutathmini hali ya tasnia hiyo na kutatua changamoto zake.
Ametoa pia wito kwa waandishi wa habari, kuzipa kipaumbele taarifa zinazolinda maadili,kukuza uchumi na kuendeleza utamaduni wa Taifa.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali itashirikiana kwa karibu na vyombo vya habari kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa 2025, kupitia Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, na kwamba uchaguzi huo unafanyika kwa uhuru, amani,haki na uwazi.
Kwa upande wake Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi, amewataka waandishi wa habari, kwamba wasitegemee tu teknolojia ya Akili Mnemba,bali waendelee kutumia uwezo wao wa kiakili katika kuchakata na kuandaa maudhui ya habari.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gerson Msigwa, amewapongeza waandishi wa habari kwa kutekeleza majukumu yao licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali, huku akiwaasa wasikate tamaa kwani wao ni nguzo ya matumaini kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, amesema waandishi wa habari wanalo jukumu kubwa la kulinda uchumi wa Taifa, na hivyo kuwataka wazipe kipaumbele habari zinazohamasisha wananchi kujikita katika shughuli za kiuchumi.
Awali Mwenyekiti wa Maadhimisho hayo ya uhuru wa vyombo vya habari Maxence Melo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jamii Africa,akiwasilisha baadhi ya maazimio ya mijadala, amesema wadau walipendelezwa kufanyike mapitio upya ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003, ili iendane na maendeleo ya teknolojia ya Akili Mnemba.
Maazimio mengine ni pamoja na kuboreshwa kanuni za maadili ya habari,kuhakikisha usalama na ulinzi wa waandishi wa habari, hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari mwaka 2025 inasema "Athari za Akili Mnemba kwa Uhuru wa Vyombo vya Habari na Tasnia ya Habari."
TAZAMA PICHA👇👇
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi akizungumza.
Katibu Mkuu Wiazara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Greyson Msigwa akizungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda akizungumza.
Mkurugenzi wa Jamii Africa Maxence Melo akizungumza.
Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO Nchini Tanzania Michel Toto akizungumza.
Viongozi wakiwa Meza kuu wakiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye Maadhimisho ya Uhuru wa vyombo vya habari
Maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari yakiendelea

Picha za pamoja zikipigwa.