TAASISI MPYA NASIMAMA NA MAMA YAJITAMBULISHA KWA MKUU WA MKOA SHINYANGA ANAMRINGI MACHA

TAASISI MPYA NASIMAMA NA MAMA YAJITAMBULISHA KWA MKUU WA MKOA SHINYANGA ANAMRINGI MACHA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

TAASISI mpya ya nasimama na Mama Tanzania Mkoa wa Shinyanga pamoja na Kanda ya Serengeti inayounda mkoa wa Simiyu,Mara na Shinyanga,imejitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,na kumpatia cheti cha usajili wa Taasisi hiyo.
Utambulisho huo umefanyika leo Aprili 30,2025 ukiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Mkoa wa Shinyanga Zamda Shabani.

Kaimu Katibu wa Taasisi hiyo mkoani Shinyanga Renatus Nzemo, ambaye pia ni Katibu wa Kanda ya Serengeti, amesema wao ni mwamvuli wa kuisaidia jamii katika mambo mbalimbali hasa wale watu ambao wananyimwa haki na kukosa wa kuwasemea, na kwamba wao wanaingia kwenye maeneo yote na kusaidia pia watu ambao wanaathiriwa na vitendo vya ukatili.

“Taasisi hii ya nasimama na Mama kama jina lilivyo, tunasimama na mama wa aina yoyote, na wengine walizani kwa sababu mheshimiwa Rais Samia ni mama, kwamba tumekuja na dhana hiyo,lakini sisi tunasimama na mama popote pale alipo,”amesema Nzemo.
Ameongeza kuwa hawashughuliki pia na Mama peke yake, bali watu wote wasio na sauti na kuathiriwa na vitendo vya ukatili.

Amesema pamoja na mambo mengine, wanadili pia na jamii katika masuala ya ujasiriamali,kubaini fursa mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo,kutoa elimu katika mambo ya afya na utunzaji wa mazingira.
“Taasisi yetu inafanya pia kazi ya kuwajengea uwezo watu kwenye eneo ambalo kama wamebaini kuna changamoto Flani ambayo inawakwamisha na kuitatua,”amesema Nzemo.

Katika hatua nyingine, amesema wanahamasisha vijana na wanawake kuchangamkia fursa za kiuongozi hasa kwenye kipindi hichi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amesema ameipokea taasisi hiyo,na kwamba dhamira na malengo yao yana manufaa makubwa kwa taifa.

Amesema wakitekeleza malengo yao kwa nia ya dhati kabisa, ana amini kwamba Mkoa wa Shinyanga utakuwa umepata ongezeko la Taasisi nzuri ambayo itasukuma gurudumu la maendeleo.
Amesema pamoja na Azima yao kubwa ya kuelezea kwamba wanasimama na mama kwa namna yoyote ile, lakini heshima hiyo ya Mama imeongezewa uzito na Rais Samia Suluhu Hassan, na kwamba Watanzania hawapaswi kuwa na shaka juu ya uwezo wa wanawake katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.

Aidha,amewashauri kwamba katika eneo la utetezi la wanawake ,vijana na makundi maalumu, kwamba waongeze pia na wanaume,sababu wamekuwa wakisahaurika na kukosa watu wa kuwasemea kutokana na wao wamekuwa wakinyanyaswa na wake zao.
Amewasisitiza pia wakahamasishe wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ambalo litaanza mwezi mei mkoani humo kwa muda wa siku saba, ili wapate fursa ya kupiga kura siku ya uchaguzi.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza.
Kaimu Katibu wa Taasisi nasimama na Mama Mkoa wa Shinyanga Renatus Nzemo akizungumza.
Mwenyekiti wa Taasisi nasimama na Mama Mkoa wa Shinyanga Zamda Shabani akizungumza.
Kaimu Katibu wa Taasisi nasimama na Mama Mkoa wa Shinyanga Renatus Nzemo (kushoto)akimkabidhi barua ya utambulisho wa Taasisi hiyo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.
Kaimu Katibu wa Taasisi nasimama na Mama Mkoa wa Shinyanga Renatus Nzemo (kushoto)akimkabidhi Cheti cha usajili wa Taasisi hiyo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.
Kikao cha utambulisho kikiendelea.
Picha za pamoja zikiendelea kupigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464