VIONGOZI SHIRIKIANENI PAMOJA KUZALISHA NA KUINUA ZAO LA PAMBA: RC MACHA
USHETU.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewaagiza wakulima wa zao la pamba, Maafisa Ugani Kilimo, Viongozi wa AMCOS, na wasimamizi wa Programu ya Kuboresha Kilimo (BBT) kushirikiana pamoja ili kuzalisha pamba iliyo bora kwa wingi kwani itarudisha thamani na heshima ya zao hapa mkoani Shinyanga.
RC Macha ameyasema hayo leo tarehe 30 Januari, 2025 wakati amewatembelea wakulima wa zao la pamba Kata ya Kisuke iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara yake ya siku 2 wilayani Kahama ambapo ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita @mbonimhita, Bi. Hadija Kabojela ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Ushetu, Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani pamoja na wataalam mbalimbali.
“Ninawapongeza kwa jitihada zenu mnazozifanya katika uzalishaji huu wa zao la pamba, lakini ninawaomba sasa muendelee kushirikiana na wataalam wetu pamoja na viongozi wote katika kila hatua ili tufanikiwe kuzalisha zaidi pamba iliyo bora kadiri iwezekanavyo ili tuweze kurudisha heshima na thamani ya Mkoa wetu,” amesema RC Macha.
Kando na hayo, RC Macha ameonekana kuridhishwa na kazi zinazofanywa na wakulima katika kufufua na kuinua upya zao la pamba na anaamini kuwa kwa msimu huu mavuno yataongezeka zaidi kutokana na elimu, usimamizi na ufuatiliaji uliofanyika.
Aidha, DC. Mboni Mhita amesema kuwa, wanaendelea kufanya tathmini na jitihada za uzalishaji wa zao la pamba ili kuhakikisha zinaleta tija na kufanya uzalishaji uongezeke jambo ambalo litapelekea kutafsiri vema maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kiasi kikubwa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Cherehani amemshukuru RC Macha kwa ziara hii kwani imewaimarisha na kuwakumbusha wakulima kuona umuhimu wa kulima pamba kwa kuzingatia utaalamu na kutumia viuatilifu ili wapate pamba nyingi yenye ubora zaidi na kukuza uchumi wao na kuongeza pato la Taifa.
RC Macha amnehitimisha ziara hii kwa awamu ya kwanza kwa kuwambusha viongozi wa Kata na Vijiji pamoja na wataalam kuweka tabia ya kuwatembelea na kuzungumza na wakulima kuhusu mafanikio, changamoto na kuweka mikakati ya kukuza ustawi wa zao la pamba katika Mkoa wa Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464