HALMASHAURI YA MANISPAA YA SHINYANGA YAENDESHA MAFUNZO YA MIKOPO YA 10% KWA KAMATI ZA HUDUMA ZA MIKOPO NGAZI YA KATA.
Na. Shinyanga MC
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeendesha mafunzo ya mikopo ya asilimia 10% inayotolewa na serikali kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu walemavu.
Mafunzo haya yamefanyika leo Oktoba 1,2024 katika ukumbi wa mikutano Shule ya Msingi Buhangija Manispaa ya Shinyanga, Mafunzo yaliyowajumuisha watendaji wa kata,maafisa elimu,Maafisa kIlimo,polisi kata, maafisa watendaji wa kata kutoka kwenye kata zao.
Awali akifungua mafunzo haya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mwl. Alexius Kagunze amewataka wanakamati hao kusimamia vyema kusajiliwa kwa vikundi hivyo ili wawezi kunufaika
“Kwa manispaa yetu tayari serikali imeshaleta fedha kwa ajili ya kusaidia makundi haya, rai yangu kwenu ninyi wasimamizi nendeni mkasimamie vyema kusajiliwa kwa vikundi vyenye sifa ya kupata mkopo.” amesema Mwl. Kagunze.
“Lengo la Serikali ni kusaidia makundi haya kujikwamua kiuchumi na kupambana na umasikini,Serikali ilisitisha utoaji wa mikopo hii kwa sababu ilikua inatolewa mikopo si kwa usahihi, sasa basi mkiwa ndio watendaji na wasimamizi wa vikundi hivyo nendeni mkafanye kazi kwa uadilifu,pamoja na weredi.” ameongeza Mwl. Kagunze.
Kwa upande wake Mkuu wa divisheni ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga Ndg. Peres Kamugisha amesema waombaji wa mkopo lazima wawe raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na kuendelea,wawe ni kikundi cha kuanzia watu watano na kuendelea isipokuwa kwa watu wenye ulemavu ambao watatakiwa wawe kuanzia wawili(2).
0 Comments