RC MACHA ALITAKA JESHI LA JADI SUNGUSUNGU KUFUATA SHERIA KANUNI NA TARATIBU ZA NCHI KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAKE
Na. Paul Kasembo, USANDA.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amelitaka Jeshi la Jadi Sungusungu Wasalama kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi wanapokuwa wanatekeleza majukumu katika maeneo yao huku akisisitiza kuacha kabisa tabia ya kuwa wanawatenga wenzao ikiwa ni sehemu ya moja kati ya adhabu zao.
RC Macha akiwa ameongozana na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni ameyasema haya leo tarehe 28 Septemba, 2024 katika kusanyiko lao linalokadiriwa kufikia watu 1000 ambalo limefanyika Kijiji cha Manyanda, Kata ya Usanda, Tarafa ya Samuye katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambapo pamoja na mambo mengine amewataka sungusungu kuwa sehemu ya kupambana na kukemea aina yoyote ya ukatili miongoni mwa jamii yetuna kuzuia mmomonyoko wa maadili kwa vijana wetu.
"Niwatake Jeshi la Jadi Sungusungu Wasalama mhakikishe kuwa mnatekeleza wajibu na majukumu yenu ya kila siku kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi, lakini acheni kabisa tabia ya kuwatenga wananchi ikiwa kama sehemu ya achabu zenu kwao na pia muwe sehemu ya wanaopambana na mmomonyoko wa maadili kwa vijana na kuzuia kwa nguvu zote aina yoyote ya ukatili mwiongoni mwetu," amesema RC Macha.
Aidha amesisitiza pia umuhimu wa kila sungusungu kando la kazi hii lakini kuwa na shughuli nyingine ya uzalishaji mali kwa kila mmoja, na kwamba kuna taratibu zitafanywa ili kujua idadi halisi ya vijana na shughuli zao ili iwe rahisi namna ya kukwamuana.
Naye mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Balozi Rajabu Omary ambaye pia Mshauri wa Rais katika masuala ya Siasa na Jamii amesema kuwa Mhe. Rais anatambua na kuthamini uwepo wa sungusungu na ndiyo maana katika utawala wake ameresha kundi hili katika jamii, huku Mwenyekiti wa Makundi ya Kijamii Tanzania ndg. Idi Ame ak8sema kuwa upo mpango wa kuanzisha mashindano ya sungusungu katila ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa ili kupata mshindi ambaye atapewa zawadi kubwa lengo ni kuimarisha Jeshi la Jadi Sungusungu.
Awali akitoa salamu kwa niaba ya sungusungu wa Mikoa ya Shinyanga, Tabora, Simiyu na Mwanza Mratibu na Kamanda Mkuu wa Sungusungu Mkoa wa Shinyanga ndg. John Kadama amesema kwamba lengo la kusanyiko hili ni kuhamasisha vijana zaidi ya 500 katika Kijiji cha Manyanda kujiunga na sungusungu ili waweze kuwa sehemu ya kulinda raia na mali zao jambo ambalo litaimarisha amani, utulivu na uchumi kwani wananchi watakuwa na usalama wakati wote.
Kusanyiko kama hii ni muendelezo ambapo ilikwishafanyika Kijiji cha Nyamilama Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Malampaka Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Busangi Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Itunduru Wilaya ya Igunga mkoani Tabora na leo hapa Manyanda Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga lengo ni lilelile kutoa hamasa kwa vijana.
0 Comments