SERIKALI NA WiLDAF KUSHIRIKIANA KUTOKOMEZA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO SHINYANGA.
Na. Paul Kasembo, SHY RS,
KATIBU Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) wamejipanga kutoa Mafunzo kwa Wazazi na Walezi Mkoani Shinyanga kwa lengo la kupunguza na kutokomeza ukatili wa kijinsia unaofanywa kwa Wanawake na Watoto huku akielezwa kuwa kwa miaka ya nyuma Mkoa wa Shinyanga ulikuwa ni miongoni mwa Mikoa inayoongoza kwa Unyanyasaji wa Kijinsia hususani ndoa za utotoni.
Ameyasema haya leo tarehe 30 Septemba 2024 alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kikao cha kupokea maoni ya kuboresha mpango mkakati wa Mkoa awamu ya pili katika kuzuia ukatili kwa wanawake na watoto kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na wataalam, wadau mbalimbali akiwemo Bi. Joyce David Kessy kutoka Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) na UNFPA.
"Pamoja na kuwapongeza kwa kuja na mpango huu mkakati awamu ya pili wa kutoa maoni juu ya namna bora ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto Mkoa wa Shinyanga, niwatake sasa mtumie vema kikao hiki na mjadili kwa kutanguliza mbele maslahi mapana ya wananchi wetu tunaowawakilisha hapa ili maoni haya yakalete tija iliyokusudiwa na Serikali," amema CP Hamduni.
Akizungumza katika kikao hicho Bi Joyce amesema, maboresho haya ya mpango mkakati wa Mkoa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto yanafanyika kupitia mradi wa CHAGUO LANGU HAKI YANGU unaotekelezwa na Shirika la WiLDAF kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland.
Ukatili wa kijinsia kwa jinsi zote umekuwa ukipingwa na kukemewa na Serikali, viongozi, mashirika ya umma, binafsi, makundi mbalimbali huku ikitajwa kuwa ni vita endelevu ambapo leo Serikali ya Mkoa wa Shinyanga na wadau mbalimbali wakiongozwa na CP. Hamduni wamefanya kikao chao cha kutoa na kupokea maoni ya namna bora ya kuboresha Mpango Mkakati wa Mkoa Awamu ya Pili katika Kuzuia Ukatili kwa Wanawake na Watoto.
0 Comments