JESHI LA POLISI SHINYANGA LINAWASHIKILIA WAHAMIAJI HARAMU 13, HUKU 11WAKILAZWA HOSPITALI YA MANISPAA YA SHINYANGA WAKIWA HOI BAADA YA KUKOSA CHAKULA
RPC Janeth Magomi.
JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia wahamiaji haramu 13 kutoka nchini Ethiopia, huku 11 wakiwa hoi na kulazwa katika hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, baada ya kutelekezwa kwenye pango huko kijiji cha Wishiteleja wilayani Kishapu na kukosa chakula.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, ametoa taarifa hiyo jana wakati akizungumza na vyombo vya habari.
Amesema wahamiaji hao haramu wamewakamata Agosti 8 mwaka huu majira ya saa 12 jioni, katika kijiji hicho cha Wishiteleja, mara baada ya kupewa taarifa na raia wema, na walipofika waliwakuta wakiwa katika hali mbaya kutokana na kukosa chakula.
“Wahamiaji hawa walikuwa wamejificha katika pango na tulikuta mikate ikiwa imeoza pamoja na maji, ikiimaanisha kwamba walikuwa wakiishi kwa kunywa maji na kula mikate, na hali zao kiafya zilikuwa mbaya sana,”amesema Magomi.
Amesema wahamiaji hao 11 bado wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya manispaa ya Shinyanga na hali zao kiafya zinaendelea kuimarika, huku wawili wakiwa kabidhi idara ya uhamiaji kwa ajili ya taratibu zingine za kisheria.
Amesema Jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi ili kubaini mtu ambaye amewaletea wahamiaji hao haramu, na kwamba hawawezi kuingia nchini Tanzania bila ya kuwa na mwenyeji, huku likitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za wahalifu na wahamiaji haramu.
Mmoja wa wahamiaji hao haramu akizungumza wakiwa hospitalini akipatiwa matibabu amesema walikuwa wanatoka nchini Ethiopia wakielekea Afrika kusini kutafuta kazi.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Wahamiaji haramu kutoka nchini Ethiopia wakiwa hospitali ya Manispaa ya Shinyanga wakipatiwa matibabu.
0 Comments