Shule iliyositisha masomo na kuwa makazi ya wananchi walioathirika na Kimbunga Hidaya
NA HADIJA OMARY, LINDI.
Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha tarehe 04 Mei 2024 kama ilivyotabiliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa saa 36 mfululizo ilisababisha maafa makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi huku wengi wao waliofikwa na maafa hayo wakijikuta wamekosa makazi, malazi na hata chakula.
Kijiji cha Mchakama kilichopo Wilayani Kilwa ni miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na athari hizo za mafuriko ambapo zaidi ya kaya 400 zimekosa makazi huku wananchi1000 wakilazimika kuishi katika vyumba vya Madarasa vya Shule ya msingi Mchakama.
Hali hiyo ya vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Mchakama kutumika kama makazi kwa wananchi hao imesababisha wanafunzi zaidi ya 200 wanaosoma shuleni hapo kulazimika kukatisha masomo yao.
Mohamedi Mwadini ambae ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mchakama alisema shule hiyo inajumla ya Wanafunzi 291 ambao kati yao 138 ni wasichana na 153 wavulana wakijumuisha wanafunzi wa Darasa la Awali mpaka Darasa la saba.
“kati ya hao wanafunzi wa darasa la awali 43, darasa la kwanza55, lapilli 34, latatu 34, lanne 27, la tano 24, la sita 27na la saba 47 ambapo 52 kati yao wakiishi upande wa pili wa kijiji (ng’ambo) ambapo kutokana na moto kujaa maji hawana uwezekano wa kuvuka upande wa pili ambako shule ilipo” alisema Mwl. Mohamed
Aliongeza kwa kueleza kuwa ni siku ya saba tangu maafa hayo yalipotokea na Wananchi walioathirika na mafuriko kukosa makazi na kuhamia katika Shule hiyo ambapo kwa sasa wanafunzi wa Shule hiyo wamelazimika kusitisha masomo yao na kuziacha familia zikiishi katika madarasa ya Shule hiyo.
" kama Wananchi hawa wataendelea kubaki hapo kwa muda mrefu wanafunzi wataendelea kukosa masomo na pengine hata kiwango chao cha ufaulu kikashuka" alizidi kueleza Mwl. Mohamed
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Mchakama Mussa Abdallah Mussa amesema baada ya mafuriko hayo kutokea jumla ya wakazi 1000 makazi yao yameharibika ikiwa ni pamoja na kupoteza mali zao, vyakula na malazi.
Alisema kati ya watu hao 1000 waliokutwa na Athari za mafuriko watu 600 kati yao wamelazimika kujihifadhi katika shule hiyo ya Mchakama kama Sehemu yao ya Makazi ya muda.
"Kijiji cha Mchakama ni kijiji cha asili watu hawakujikusanya pamoja hivyo Mto huu umegawanyisha tuna kambi mbili ambazo zinawananchi 500 wakiwemo na hao wanafunzi mpaka sasahivi hawana huduma yoyote ya kijamii hawana chakula, hawapati matibabu na hata masomo kwa wanafunzi na hawawezi kuja huku kwa maana maji ni mengi".
"Jingine wananchi hawa waliopata Maafa tumewaweka pale katika vyomba vya madarasa kutokana na ukosefu wa maeneo na tunafahamu hivi karibuni mitihani ya mihula itaanza siku si nyingi hivyo ili kuwapisha wanafunzi hawa kuendelea na Masomo tunaiomba Serikali kutupa maeneo pamoja na Mahema yatakayotuwezesha kuishi kwa muda huku wanafunzi hao wakiendelea kusoma".alisema Mussa.
Asia Josephat ni mzazi wa mwanafunzi Zuhura Hassan anaesoma Darasa la kwanza katika shule hiyo ya msingi Mchakama amesema baada ya mafuliko hayo kutokea miongoni mwa vitu vilivyosombwa ni pamoja na vifaa vya shule vya watoto.
" kwa hivyo hapa hata shule itakapofunguliwa na watoto kuruhusiwa kuendelea na masomo bado watoto wetu wanachangamoto za vifaa vya shule hivyo tunaiomba Serikali kutusaidia vifaa hivyo ili Wanafunzi hao watakaporuhusiwa kurudi shuleni waweze kuendelea na Masomo " alisema Asia
"Lakini si hilo tuu sasa hivi ni muda wa magonjwa ya mlipuko tunapokusanyika watu wengi kwa wakati mmoja sehemu moja inakuwa ni rahisi kuingia ugonjwa ukizingatia hapa pia tunaishi na watoto wadogo wa miaka miwili, mitatu na kuendelea kwa hivyo mi niiombe serikali kwa muda huu mfupi hata kama tungeletewa maturubai ilimradi tukapisha hapa shuleni wanafunzi wakaendelea na shule maana kwa sasa hivi imejifunga uwezi kuwaambia wanafunzi waje hapa kwa sababu madarasa yote ndo tumefanya majumba ya watu” aliongeza kusema Asia
Akizungumza Bungeni Alhamisi ya Mei 9 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema maeneo ya Kilwa na Mtwara yalirekodi kiwango kikubwa cha mvua zilizotokana na kimbunga Hidaya. Kwa kawaida, wastani wa mvua kwa kituo cha Kilwa ni milimita 96.6 na kwa kituo cha Mtwara ni milimita 54.
Alisema hata hivyo, kuanzia Mei 3 hadi 4, 2024, jumla ya milimita 316 za mvua zilipimwa katika kituo cha Kilwa, sawa na asilimia 327 ya kiwango cha mwezi huku upande wa Mtwara, jumla ya milimita 99 zilipimwa katika muda huo ambazo ni sawa na asilimia 183 ya kiwango cha mwezi.
“Kwa hali ya kawaida, mvua ya milimita 316 iliyonyesha Kilwa kwa saa 36 tu, ni sawa na mvua ya miaka mitatu kwa mwezi Mei, yaani Mei 2024, Mei 2025 na Mei 2026”
Hiki ni kiwango kikubwa sana na ndiyo maana kumekuwa na madhara makubwa ya uharibifu wa miundombinu mbalimbali” alisema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Mei 1, 2024 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa taarifa ya uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi mashariki mwa Pwani ya Mtwara ambapo mifumo ya hali ya hewa iliyopo ilionesha kuwa mgandamizo huo mdogo wa hewa ulitarajiwa kuimarika na kufikia hadhi ya kimbunga kamili siku ya Mei 2, 2024.
Taarifa ya Mamlaka hiyo ilieleza wakati mgandamizo huo mdogo wa hewa ukiendelea kuimarika, ulitarajiwa kusogea kuelekea baadhi ya maeneo ya Pwani ya Tanzania ikiwamo Mkoa wa Lindi kuanzia usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa Mei 3, 2024 na kuendelea kuwepo katika maeneo ya ukanda huo hadi Mei 6,2024 kisha kukadiriwa kupungua nguvu baada ya Mei 6, 2024.
Uwepo wa mgandamizo huo mdogo wa hewa ulitarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dar es salaam na maeneo ya jirani hivyo Wananchi walishauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya Wataalamu katika Sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
0 Comments