Header Ads Widget

GEF YATOA ZAIDI BILIONI 4/- KWA CSOs 44 KUTEKELEZA MIRADI YA UHIFADHI MAZINGIRA


GEF kupitia UNDP yatoa zaidi ya shilingi 4 .04 bilioni kwa CSOs 44 nchini kutekeleza miradi ngazi ya jamii.

Mwandishi wetu,Dar es Salaam

Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) kupitia Programu ya Ruzuku Ndogo inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesaini makubaliano ya kutoa sh 4.04 bilioni kwa mashirika yasiyo ya kiserikali 44 nchini ili kutekeleza miradi ya Uhifadhi wa Mazingira, Misitu, kuendeleza ufugaji nyuki, kutunza vyanzo vya Maji na uwezeshaji Jamii kiuchumi.

Utiaji saini wa Makubaliano hayo umefanyika leo April 4,2024, katika Makao Makuu ya Jengo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania na kuongozwa na Mwakilishi Mkaazi wa UNDP ndugu Shigeki Komatsubara.

Miongoni mwa mashirika yaliyosaini mkataba kupatiwa fedha hizo ni shirika la Wanahabari wa jamii za pembezoni(MAIPAC) ambalo limekuwa likitekeleza miradi ya uhifadhi wa mazingira,Misitu na vyanzo vya maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa maarifa ya asili.

Akizungumza katika hafla hiyo, Komatsubara amesema kuwa mashirika zaidi ya 400 yalituma maombi kuomba fedha za kutekeleza miradi midogo midogo nchini Tanzania bara na Zanzibar lakini ni mashirika 44 tu ndio yamefanikiwa.

"Hongereni sana leo kuwa miongoni mwa mashirika na asasi ambazo zimepata fursa kutekeleza miradi midogo Tanzania.

Komatsubara amesema anaimani kubwa mashirika ambayo yanapewa fedha hizo yatakwenda kutekeleza vyema miradi ambayo itagusa jamii hasa wanawake,vijana,walemavu na jamii za pembezoni.

"Tunatarajia miradi yetu itakwenda kuchochea maendeleo katika jamii ikiwepo pia kukabiliana na vichocheo vya uharibifu wa mazingira" amesema

Naye Mwakilishi kwa niaba ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Lilian Lukambuzi akizungumza katika hafla hiyo alitaka mashirika yaliyopewa fedha hizo kuzitumia kama ilivyokusudia.

Amesema serikali itafuatilia miradi ambayo inakwenda kutekelezwa ili kuhakikisha inakuwa na tija.

Awali Mratibu wa Programu ya Ruzuku Ndogo za GEF nchini, ndugu Faustine Ninga amesema haikuwa kazi rahisi kupitisha mashirika hayo machache kupata ruzuku kutokana na uhitaji mkubwa kutoka katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kamati ya Uendeshaji ya programu hiyo ya Ruzuku Ndogo za GEF ambayo inaundwa na wataalam kutoka sekta mbalimbali na taasis zisizo za Kiserikali kwa kushirikia na UNDP ilifanya kazi kubwa ya kuchambua maandiko ya miradi zaidi ya 400.

Hata hivyo,amesema kutokana na uhitaji kuwa mkubwa ni mashirika 44 tu ndio yalipitishwa, ijapokuwa mashirika mengine yalikuwa na madokezo mazuri ya miradi.

Hata hivyo ameyataka mashirika haya kufuata kanuni na taratibu za nchi na miongozi ya uendeshaji wa taasisi zisizo za kiserikali katika utekelezaji wa miradi yao ili miradi iwe na matokeo mazuri.

Amesema kamati ya ufuatiliaji miradi hiyo itakagua na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ili kuhakikisha kuwa jamii zinanufaika .

Wakizungumza baada ya kusaini mikataba baadhi ya watendaji wa mashirika hayo walipongeza UNDP kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi midogo katika jamii.

Mkurugenzi wa shirika la MAIPAC Mussa Juma alisema hii ni mara ya pili shirika hilo kupata fedha na kueleza katika miradi iliyopita kulikuwa na matokeo mazuri.

"Tulikusanya maarifa ya asili katika uhifadhi mazingira,misitu na vyanzo vya maji na kufanikiwa kutengeneza kitabu cha kwanza nchini cha umuhimu wa maarifa ya asili ambacho kilizinduliwa na Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dk Seleman Jafo na kugawanywa bure katika shule,taasisi za serikali na binafsi"alisema

Alisema pia waliweza kushirikisha watungaji wa sera kutambu umuhimu wa kulinda na kuendeleza maarifa ya asili ikiwepo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

"Safari hii maarifa ya asili yatakusanywa na kuhifadhiwa katoka vitabu na katika vyombo vya habari kwa jamii ya Wahdzabe na waberbeig lakini pia vyanzo vya maji vitahifadhiwa"alisema

Clara Chuwa mratibu miradi wa Shirika la WODSTA alisema wanakwenda kutekeleza Mradi kwa ajili kuwezesha kutunza mazingira na matumizi endelevu ya msitu na chanzo Cha maji kijiji Cha lemanda, Kata ya oldonyosambu,wilaya ya Arumeru.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la SECCA ,Esaya Yusufu alisema wanakwenda kutekeleza mradi wa upandaji miti na kuchimba kisima katika eneo la ikolojia ya serengeti.

Mfuko wa mazingira Duniani(GEF) ulianzishwa mwaka 1992 na umekuwa na miradi katika nchi 136 Duniani.

Orodha ya mashirika yaliyopita kutekeleza miradi ni hii

Post a Comment

0 Comments