Header Ads Widget

MANISPAA YAANZA MSAKO WATOTO AMBAO HAWAJAANDIKISHWA DARASA LA AWALI




 Viongozi wakikagua uandikishaji wa darasa la Awali

Na Kareny Masasy

MANISPAA  ya Shinyanga  imeanza msako  nyumba kwa nyumba  na  kwenye vituo vya kulea watoto (daycare centre)  kwa watoto ambapo hawajaandikishwa darasa la awali  wamefikia umri wa miaka mitano.

Manispaa hiyo mpaka sasa mwezi Marchi  uandikishaji umefikia asilimia 85 huku lengo likiwa asilimia 100.

Wakazi wa manispaa ya Shinyanga  akiwemo  Gidion  Juma anasema  mtoto wake ana umri wa miaka mitano ameona ampeleke kituo cha kulea watoto kwani shule iko mbali hofu iliyopo kupotea hakuna wa kumfuata.

Pia Rahel  Moses anasema  ameamua kumpeleka kituo cha kulea watoto  sababu yupo  mtu wa kushinda naye na analipa pesa kidogo akiwa shuleni atatoka saa nne nyumbani atakuwa pekeyake.

Naye Dolnad Kiula anasema  wapo wazazi kwa makusudi hawawapeleki watoto kuanza shule  bila sababu za msingi  suala la msako kila nyumba ni zuri na watakao bainika wachukuliwe hatua.

“Jamani naona kama viongozi wanahangaika na wazazi kwani  wanaokaidi  iwepo sheria ndogo  kuwa adhibu ili watoto wapate haki yao ya elimu”anasema Kiula.

Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la  Invest Children Societies  (ICS) mkoa wa Shinyanga Sabrina Majikata anasema umuhimu wa darasa la awali ni kumuandaa mtoto katika ujifunzaji wa maendeleo katika ukuaji wake  na kituo cha kulelea watoto ni kucheza kwa kadri ya umri wa mtoto kuanzia miaka miwili hadi minne.

“Mtoto anapozaliwa tu ubongo wake  unakuwa umefikia asilimia 25 katika ukuaji wake na anapofikisha umri wa miaka mitano unakuwa   kwa asilimia 92 hivyo   darasani anaendelea kujifunza  zaidi  vitu mbalimbali kupitia nyimbo na michezo”anasema  Majikata.

Majikata anasema mtoto anatakiwa kuanzishwa darasa la awali akiwa na umri wa miaka  mitano na akifikisha umri wa miaka sita aanze darasa la kwanza lakini mzazi analazimisha  huko  kwenye vituo aanze pia kufundishwa kusoma na kuandika.

“Mzazi unaposhindwa kumpeleka mtoto shule umri unaotakiwa  tayari umeanza kumnyima haki yake ya elimu ambayo anatakiwa kuipata akiwa mdogo”anasema Majikata..

Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Mwenge  Alex Malya anasema  shule hiyo inaongoza kuwa na wanafunzi wengi wa darasa la awali   changamoto iliyopo ni walimu wa kuwafundisha na madarasa ya kuwaweka ni machache.

“Darasa moja linawanafunzi  zaidi ya wanafunzi 100 na Mwalimu ni mmoja hivyo bado kunachangamoto ya uangalizi wa watoto  ingawa walimu wamekuwa wakijitahidi kwenye hilo”anasema Malya.

Malya anasema sababu ya wingi wa watoto kwenye shule hiyo iko mjini na kila mzazi anataka kuleta hapa  ingawa kata wanazoishi kuna shule mikakati iliyopo mwakani  malengo yaliyoweka yatakuwa hayo hayo hawatazidisha watoto.

Sera ya elimu ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016  inaeleza darasa la awali kuwa Mwalimu mmoja  na wanafunzi 25 tu.Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mwenge  Hemed  Hussein anasema Mwitikio wa darasa la awali kwa shule hiyo umekuwa mzuri  sababu maoteo kwa mwaka huu yalikuwa wanafunzi 130 na mwezi Januari idadi hiyo ilikuwa imetimia.

“Wazazi waliendelea kuleta watoto wao kutoka maeneo mbalimbali mpaka wamefika wanafunzi 287 wa darasa la awali  na darasa moja lina wanafunzi zaidi ya 100”anasema Hussein.

Kaimu ofisa elimu manispaa ya Shinyanga  Grace Kuzanza anasema  shule ya mwenge wazazi wengi wamekuwa ndiyo kimbilio lao na shule zingine zina wanafunzi wachache.

Kuzanza anasema  bado mwitikio wa wazazi katika uandikishaji wa darasa la awali ni mdogo  ikiwa Maoteo ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali  kwa mwaka 2024 ni wanafunzi  5947  wasichana 3000 na wavulana 2,947

Kuzanza anasema  kuanzia mwezi Oktoba 2023  hadi March 2024  wanafunzi walioandikishwa  ni 5059  wavulana ni 2457 na  wasichana ni  2602 wakiwemo  walemavu wasichana watatu na wavulana wanne  sawa na asilimia 85 .

“Bado baadhi ya wazazi  hawapeleki watoto wao kuanza darasa la awali  hata kama umri unaruhusu kuanza anasubiri kumuanzishia moja kwa moja darasa  la kwanza”anasema Kuzanza.

Kuzanza anasema uandikishaji wa darasa la awali kwa mwaka jana ulifikia asilimia 105 kwa  kufikia mwezi March lakini  kwa mwaka huu umefikia asilimia 85  zoezi linalofanyika kuwasaka watoto wote kwenye vituo vya kulea watoto wenye umri wa miaka mitano ili waanze darasa la awali.

Kwa Mujibu wa  Sheria  ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 na sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka ya Mwaka 2008  ni kuhakikisha mtoto anaandikishwa shule na kufuatilia maendeleo yao kwa kuwapatia mahitaji yote ya shule.

Katika Programu Jumuishi ya Taifa ya Maendeleo ya Awali ya Mtoto  PJT-MMMAM inaeleza Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwenye elimu ya awali kuifanya kuwa ya lazima.

Katika sera ya elimu na mafunzo  ya mwaka  2014  na maboresho yake ya mwaka 2016 kuwa elimu bila malipo na kujumuisha elimu ya msingi   kuzita shule zote  kuwa na darasa la elimu ya awali kwa watoto wenye  umri wa miaka mitano.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments