Header Ads Widget

SHIRIKA LA AGAPE LINAVYOPITIA MAGUMU UKOMBOZI MTOTO WA KIKE KIELIMU

SHIRIKA LA AGAPE LINAVYOPITIA MAGUMU UKOMBOZI MTOTO WA KIKE KIELIMU

"Watoto wa kike wenye akili ndio wanaopewa mimba za utotoni na kuozeshwa,30 awarudisha nyumbani kwao"

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

SHIRIKA la AGAPE ambalo lilianzishwa mwaka 2009 mkoani Shinyanga, limekuwa na mchango mkubwa hapa chini katika kumkomboa mtoto wa kike kielimu na kutimiza ndoto zao,ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni.
Shirika hilo limekuwa likisaidia watoto wakike ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili ikiwamo kupewa ujauzito na wengine kuozeshwa ndoa za utotoni na kuzima ndoto zao,ambapo huwaibua na kuwarudisha darasani na kuendelea na masomo kwa mfumo usiyo rasmi na kutimiza ndoto zao.

Mkurugenzi wa Shirika hilo la Agape John Myola, amebainisha hayo leo Desemba 30,2023 wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hii, walipotembelea katika shule ya Agape Open Knowledge iliyopo Chibe Manispaa ya Shinyanga.
Amesema Shirika hilo baada ya kuwakomboa watoto wa kike ambao baadhi wamepewa ujauzito na wengine kuozeshwa ndoa za utotoni, ndipo wakaona ni vyema kuanzisha shule ambayo itakuwa ikitoa elimu kwa mfumo usiyo rasmi ili watoto hao waendelee na masomo na kutimiza ndoto zao.

Anasema watoto hao wanapokaribia kufanya mtihani ya kuhitimu hua wanawatafutia kituo cha kufanyia mitahani yao, na kumshukuru Mungu wamekuwa wakipa ufaulu mzuri na wengi hadi sasa wapo Vyuo Vikuu na wengine walishamaliza na wanakazi zao.
“Watoto hawa wanaakili sana hua wanapata ufaulu wa juu tu, ukiangalia hata matokeo ya wanafunzi wetu ambao wamemaliza Kidato cha Sita Ufaulu wao ni daraja la kwanza, lapili, na wote hadi sasa wapo JKT,”amesema Myola.

“Wanafunzi ambao wamemaliza Chuo Kikuu mwaka huu, wapo 6 na wamesomea Uhasibu, Sheria, Elimu na Masuala ya Jinsia, na kuna wanafunzi wengine 21 bado wapo vyuo wakiendelea na masomo yao, na wengine kidato cha 6,5 na 4 na wanafanya vizuri, sijui kwanini watoto wenye akili ndiyo wanapewa hizi mimba za utotoni na kuozeshwa,”ameongeza Myola.

CHANGAMOTO

Katika hatua nyingine Myola, ametaja Changamoto ambazo wanazipitia kwa sasa katika ukombozi wa mtoto wakike kielimu, kuwa ni ukosefu wa chakula hali ambayo ilimlazimu watoto 30 kuwarudisha majumbani mwao, kutokana na kushindwa kuwahudumia chakula na kubaki na watoto 27.

Anasema tatizo la chakula ndiyo limekuwa likimuumiza kichwa kutokana na kukabiliwa na ukata wa fedha, na kuwaomba wadau pamoja na Serikali kumshika mkono kumpatia chakula, ili aendelee kuwahudumia watoto hao katika kutimiza ndoto zao ambazo zilitaka kuzimwa sababu ya kupewa ujauzito na wengine kuozeshwa ndoa za utotoni.
“Namshukuru sana Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi amekuwa na msaada mkubwa kunisaidia upande wa chakula hata majuzi tu hapa kwenye Sikukuu ya Kristmas kanipatia chakula, Mungu ambariki sana anaguswa na mtoto wa kike apate elimu,”amesema Myola.

MIKAKATI YA AGAPE

Aidha, ametaja mikakati ya Agape katika kukabiliana na janga hilo la chakula, kwamba wameanzisha Kilimo cha Mahindi Hekali 5, pamoja na kutarajia kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji msimu wa kiangazi sababu Kisima cha Maji wanacho, lakini Pampu yake ni mbovu nakuomba msaada kwa wadau wawasaidie kuitengeza ili wafanye kilimo hicho ambacho kitakuwa mkombozi kwao kwa chakula na hata kuinuka kiuchumi.
“Ardhi tunayo Hekali 5 na Mikakati yetu ni kuitumia ipasavyo kulima mazao mbalimbali kwa kufanya Kilimo cha Umwagiliaji, ilitukabiliane na tatizo hili la chakula pamoja na kuinuka kiuchumi kwa kulima mazao ya biashara, fedha ambazo zitatumika kusomesha watoto hawa na kuwatimizia mahitaji yao mbalimbali,”amesema Myola.

Ametaka mikakati mingine kuwa ni kuanzisha pia ufugaji wa Samaki sababu bwawa tayari wameshachimba, lakini wameshindwa kulikamilisha vizuri sababu ya ukata wa fedha, huku wakianzisha pia ufugaji wa kuku na sasa wanakuku 16, na matarajio yao ni kufikisha kuku 3,000 ili kufanya ufugaji wa kibiashara.

ELIMU YA UJASIRIAMALI

Amesema mbali na watoto hao kupatiwa elimu, pia wamekuwa wakiwafundisha udereva wa bajaji, ili watakapokuwa katika majukumu yao mengine wanaweza kujiajiri kupitia bajaji na kuondoa dhana kwamba kazi hiyo ni yawatoto wa kiume bali hata wakike nao wanaweza na kujiongeza kipato.

Nao baadhi ya watoto hao ambao majina yao yamehifadhiwa, wamelishukuru Shirika hilo la Agape kwa kukomboa ndoto zao ambazo tayari zilikuwa zimeshazimwa, kutokana na baadhi yao tayari wameshajifungua watoto lakini sasa wanaendelea na masomo.

TAKWIMU NDOA UTOTONI

Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Shirika la watoto Duniani (UNICEF) Mwaka 2012, Mkoa wa Shinyanga umetajwa kuongoza kwa tatizo la ndoa za utotoni kwa asilimia 59 ikifuatiwa na Tabora 58 ya tatu ni mara 55.

KWA MAWASILIANO YA AGAPE 0757516965,0713516965
Mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola (kushoto) akielezea magumu ambayo anapitia kwa sasa katika kumkomboa mtoto wa kike kielimu,huku akiwa amebeba Mmoja wa Mtoto ambaye amezaliwa na Mtoto mwenzie anaishi naye katika shule ya Agape iliyopo Chibe Manispaa ya Shinyanga.
Muonekano wa Shamba la Mahindi ambalo analima ili kukabiliana na tatizo la Chakula.
Muonekano wa Shamba la Mahindi ambalo analima ili kukabiliana na tatizo la Chakula.
Mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola (kulia) akielezea Kisima cha Maji ambacho wanatarajia kufanya Kilimo cha Umwagiliaji kipindi cha Kiangazi, lakini Pampu yake imekufa na kuomba msaada wa matengenezo sababu kwa sasa hali yake ya kifedha siyo nzuri.
Mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola akionyesha eneo ambalo wamechimba bwawa kwa ajili ya kuja kufuga Samaki,lakini wameshindwa kuliendeleza sababu ya ukata wa fedha.
Mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola (kulia) akielezea mikakati ya ufugaji kuku kibiashara.
Bajaji ambayo hufundishwa watoto wa kike shughuli za ujasiriamali.
KWA MAWASILIANO YA AGAPE 0757516965,0713516965.

Post a Comment

0 Comments