Header Ads Widget

UKOSEFU ELIMU YA UNYONYESHAJI SAHIHI KWA WANAWAKE CHANZO CHA UDUMAVU KWA WATOTO


Ukosefu elimu ya unyonyeshaji sahihi kwa wanawake chanzo cha udumavu kwa watoto

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Kukosekana kwa elimu sahihi ya unyonyeshaji kwa wanawake imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa tatizo la udumavu kwa watoto.

Baadhi ya wanawake mkoani Shinyanga bado hawana elimu hiyo ya unyonyeshaji na hata kusababisha tatizo la udumavu kwa watoto kuendelea.

Kwa mujibu wa utafiti wa Taifa wa masuala ya Afya na Lishe mwaka 2022, unaonyesha kuwa tatizo la udumavu kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano katika Mkoa wa Shinyanga ni asilimia 27.5 huku ukondefu ikiwa ni asilimia 4.3.

Afisa Lishe Mkoa wa Shinyanga Yusuph Hamisi, anakiri kwamba wanawake katika Mkoa wa Shinyanga bado hawana elimu sahihi ya unonyeshaji watoto, na kwamba asilimia 30 tu ya wanawake ndiyo hunyonyesha watoto wao ndani ya saa moja mara baada ya kujifungua.

Anasema maziwa ya mama kwa mtoto ni muhimu katika Afya yake ikiwamo ukuaji kimwili, kiakili, na hata kupunguza katika tatizo la udumavu.

“Mtoto akizaliwa baada ya saa moja, anapaswa kunyonyeshwa yale maziwa ya kwanza ya njano na siyo kuyakamua na kuyamwaga sababu yanavirutubisho na nikinga ya mwili ya mtoto na hayana madhara,”anasema Hamisi.

Anasema lakini wanawake wengi hua hawapendi kuwanyonyesha watoto wao maziwa hayo ya njano wakidhani ni machafu na kuwanyima kinga watoto.

Anasema kwamba mtoto akishazaliwa licha ya kunyonya maziwa hayo ya njano pia anapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya miezi sita bila ya kupewa kitu chochote wala maji, ushauri ambao umekuwa ukipuuzwa na wanawake wengi na hata kuwasababishia maradhi mbalimbali.

“Mtoto akishafikisha miezi sita ndipo anapaswa kuanza kupewa vyakula vya ziada kwa kuzingatia lishe bora kwa kufuata makundi matano ya chakula, huku pia akiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi akifikishe miaka miwili hapo lazima awe na afya njema,”anafanua Hamis.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile, anasema tatizo la udumavu kwa watoto wadogo waliochini ya umri wa miaka mitano mkoani humo limepungua kutoka asilimia 32.1 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 27.5 mwaka 2022.

Anasema udumavu huo umepungua kutokana na elimu ya unyonyeshaji na lishe ambayo imekuwa ikitolewa kwa wazazi kupitia huduma za kiafya, na kueleza kwamba bado elimu zaidi ina hitajika kutolewa hasa maeneo ya vijijini.

Mwanamke Kareny Jamsoni, anasema yeye alishapata elimu ya unyonyeshaji katika kituo cha Afya Kambarage Manispaa ya Shinyanga, na mtoto wake ambaye kwa sasa ametimiza miezi sita, hakuwahi kumpatia kitu chochote zaidi ya maziwa ya mama.

Anasema awali hakuwa na elimu hiyo ya unyonyeshaji, lakini sasa hivi elimu anayo na mtoto wake ana Afya njema na hapati maradhi ya mara kwa mara sababu ana kinga ya maziwa ya mama.

Mwanamke mwingine Khadija Shabani, anasema baadhi ya wanawake hua hawapendi kunyonyesha watoto wao kwa Imani potofu kwamba maziwa yatalala na kupoteza muonekano mzuri.

Anasema elimu bado inahitajika kwa wanawake juu ya faida ya unyonyeshaji watoto, na kuondoa imani potofu ya maneno ya mitaani kwamba wakinyonyesha maziwa yao yatalala, na hatimaye kusababisha udumavu kwa watoto wao.

“Mimi mwanzoni nilikuwa nimeathiriwa na maneno haya ya mitaani juu ya unyonyeshaji, unajua wanawake hua tunadanganyana sana, lakini nilipokwenda kujifungua mtoto wangu huyu, nilipata elimu ya unyonyeshaji na nikafuata ushauri wa wataalamu na sasa mwanangu ana Afya njema tu,”anasema Khadija.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi, anasema mtoto wake wa kwanza baada ya kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa Afya alimnyonyesha miezi sita bila ya kumpatia kitu chochote na Afya yake ni njema hadi sasa.

Anawasihi wanawake wafuate ushauri ambao hupewa na wataalamu wa Afya katika suala zima la kuzingatia Afya zao na watoto.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, anawashauri wanawake katika Mkoa huo kujenga tabia ya kujifungua katika huduma za kiafya ili wakapate elimu ya afya ya uzazi, lishe na unyonyeshaji sahihi watoto.

Anasema tatizo la udumavu kuendelea dhidi ya watoto wadogo ni ukosefu wa elimu kwa wazazi, na kutoa maagizo Maafisa lishe na Wataalamu wa Afya, wafanye mikutano ya mara kwa mara na kutoa elimu ya unyonyeshaji na lishe hasa maeneo ya vijijini.

“Naelekeza Maafisa lishe wote mkoani hapa wasikae Maofisini bali waende kutoa elimu ya lishe na uyonyeshaji kwa wananchi, sababu bila kutolewa elimu tatizo hili la udumavu kwa watoto litaendelea kuwepo hapa Shinyanga,” anasema Mndeme.

Mndeme anatoa maagizo pia fedha za lishe ziendelee kutolewa kulingana na mpango kazi uliopo ili kutoathiri utekelezaji wa shughuli za lishe, pamoja na kufanya maadhimisho ya siku ya Afya na lishe kila robo kwa mujibu wa muongozo uliopo ili kufikisha elimu ya lishe na unyonyeshaji kwa jamii.

Post a Comment

0 Comments