Header Ads Widget

MWENYEKITI SPC AIOMBA SERIKALI KUWAPA MAGARI MAZURI WAANDISHI WA HABARI WAKATI WAKIWA KWENYE ZIARA ZA VIONGOZI



Suzy Luhende,Shinyanga Blog

 Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakulu ameiomba serikali kuwapa magari mazuri waandishi wa habari wakati wa ziara za viongozi, kwani kumekuwa na tabia ya waandishi wa habari kupewa magari mabovu ambayo yanaweza kusababisha ajali ama kuharibika wakati wowote.

Hayo ameyasema leo kwenye maadhimisho ya siku ya vyombo vya habari mkoa wa Shinyanga  yaliyoandaliwa na Klabu ya waandishi wa habari mkoani hapa (SPC) na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali wa habari mkoani humo, ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme.

Kakulu amesema waandishi wa habari wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi mbalimbali katika utendaji wao wa kazi, ambapo wamekuwa wakienda kuibua habari mbalimbali, lakini baadhi ya watendaji  wamekuwa wakiwatishia na kuwaharibia vifaa vyao vya kazi,  hali ambayo imekuwa ikiwafanya wasifanye kazi zao kwa ufasaha zaidi.

"Tunaiomba serikali itusaidie sisi waandishi wa habari, kwani katika utendaji wetu wa kazi tumekuwa tukikutana na changamoto nyingi zikiwemo za kupewa vitisho, na kumekuwa na urasimu wakati wa kutoa taarifa, mwandishi anaweza kuibua habari ya madawati kutengenezwa chini ya kiwango waandishi wakiandika inakuwa shida,"amesema Kakulu.

Amesema baadhi ya watendaji hawapendi habari za kuibua, hivyo wakisikia imeandikwa habari huanza kupiga simu kwa wamiliki wa vyombo vya habari na kuanza kuwatisha kuwa watawashitaki, hivyo wameiomba serikali iziangalie hizo changamoto na kuzipatia ufumbuzi ili waandishi waweze kufanya kazi zao kwa uhuru.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi amesema kutokana na changamoto hizo amewataka maafisa habari kushirikiana na waandishi wa habari na kuhakikisha wanazichukua na kuzishughulikia changamoto hizo zinazowakabili, huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili kuhakikisha mkoa unakua na maendeleo zaidi.

Pia Samizi amewapongeza waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga kwa kazi nzuri wanayofanya katika utekelezaji wa majukumu yao, huku akiwataka kutumia kalamu zao vizuri,na watambue kuwa uandishi wa habari ni taaluma siyo utashi tu  wa kuandika, hivyo waandike habari kwa kutenda haki kwa kila mmoja.

“Waandishi wa habari wanafanya kazi nzuri ya kuhabarisha jamii, wito wangu watumie kalamu zao na matamshi yao katika kuhabarisha jamii, ili habari iliyokusudiwa iwafikie walengwa ikiwemo kuhabarisha na kuburudisha”,amesema Samizi.

Naye  meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo amewataka watoa huduma za maudhui kuhakikisha wanazingatia sheria na kuwa na leseni za utoaji huduma za mawasiliano akisisitiza kuwa hataruhusu sheria zivunjwe.

“Ndugu zangu waandishi wa habari niwaombe wale ambao wana Blogs na Online Tv ambazo hazina leseni muombe leseni, pia andikeni vizuri vichwa vya habari,  na mtumie taaluma zenu vizuri ili msijiingize kwenye migogoro, na muwe makini katika ku copy  na ku paste kwa sababu unakuta story uliyoipaste ina makosa hivyo story hiyo inasambaa kila chombo ikiwa na makosa hayohayo, na hakikisheni mnazingatia sheria za uandishi wa habari"amesema  Mihayo

Post a Comment

0 Comments