Header Ads Widget

TUNDU LISSU AILIPUA TENA SERIKALI

Lissu ailipua tena Serikali, nayo yamjibu


Kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuwa Serikali imekuwa ikiruhusu usafirishaji wa wanyama kwenda nje ya nchi tangu mwaka 1985, imeiibua Wizara ya Maliasili na Utalii ikisema hairuhusiwi mtu yeyote kusafirisha wanyama.

Akizungumza kwa njia ya simu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema siku za nyuma sheria iliwaruhusu watu kuvuna wanyama wao wanaowafugia kwenye bustani na kuamua kuwauza nje ya nchi au hata kuwachinja kwa matumizi ya kitoweo, lakini sasa hairuhusiwi.
 
Hata hivyo, akihutubia mkutano wa hadhara baada ya kuwasili nchini , Lissu alisema kuna biashara kubwa ya kuuza wanyama nje ya nchi inafanywa na Serikali na madhara yake ni kuwa siku zijazo watalii watahamia huko wanakofugwa wanyama hao.

“Emirates Sharja wamefungua shamba la wanyama, eneo hilo linalokusanya wanyama mbalimbali ndilo kubwa duniani, miti iliyopo ni zaidi ya 100,000 na wanyama zaidi ya 50,000 kutoka Afrika,” amesema Lissu.

Amedai kuwa hatua ya Serikali ya sasa kuwaondoa Wamasai ni kutoa nafasi kwa Waarabu wa Emirates kuhamisha wanyama wapeleke kwao, “unafikiri wakipeleka wanyama kwao watalii wataenda wapi?”

Hata hivyo, Profesa Sedoyeka ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema: “Hata wewe hapo unaweza kuanzisha bustani yako ukaomba mbegu za wanyama ukapewa, zamani ilikuwa hao wanyama wakizaliana unaweza kuuza au kusafirisha, lakini sio kuuza wanyama wa Serikali, kwa sasa hata wa bustani hawaruhusiwi kusafirisha.”
 
 Amesema ndiyo maana hivi sasa Serikali ina mgogoro na wafugaji ambao kwa muda mrefu wamezuiwa kusafirisha, nayo inaangalia namna ya kushughulikia jambo hilo lakini uuzaji na usafirishaji wa wanyama wa Serikali haujawahi kuruhusiwa.

Serikali ilipiga marufuku usafirishaji wa wanyama hao kwa kuwa kuna watu wasio waaminifu walikuwa wakitumia mwanya huo wa ruksa ya wafugaji kuiba wanyama wa Serikali na kuwasafirisha kinyume cha sheria za nchi.

Juni 4, 2022 Serikali iliruhusu usafirishaji wa wanyamapori hai waliokuwa wamesalia kwenye mazizi na mashamba ya wafugaji baada ya zuio lililotolewa mwaka 2016.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 4, 2022 na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), ruhusa hiyo ni kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Juni 6 hadi Desemba 5, 2022.

Hata hivyo, Waziri wa Maliasili na utalii alirejesha zuio hilo ndani ya saa 24 na kusema litadumu mpaka pale Serikali itakapoamua vinginevyo.


SOMA HAPA ZAIDI CHANZO MWANANCHI

Post a Comment

0 Comments