Header Ads Widget

WAZAZI WAPATA MWAMKO WA MAANDALIZI YA WANAFUNZI KABLA YA KUFAULU.








Baraza la watoto linaloundwa na wanafunzi wa shule za msingi kata ya Tinde halmashauri ya wilaya ya Shinyanga  wakifurahi  kwa pamoja kupinga ukatili.

Na  Kareny  Masasy,Shinyanga

WAZAZI  wa kijiji cha Nhubili  kata ya Tinde halmashauri ya wilaya ya Shinyanga  wamepata mwamko wa kufanya  maandalizi ya shule kwa wanafunzi  baada ya kipindi cha kiangazi kutunza  mifugo na kipindi cha masika kuiuza.

Wazazi  wapatao  saba wakiwemo Helena  Ngoro na  Maige Hussein wakiongea jana  kijijini hapo  kwa nyakati tofauti wamesema  walikuwa na  uhakika wa watoto wao kufaulu na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza.

Ngoro amesema  wanalima na kuuza mazao  na fedha hizo huzinunua mbuzi .kondoo au ng’ombe  na kipindi cha  masika huuza tena na kununua  mahitaji ya  shule ikiwemo baiskeli sababu wanakofaulu shule zinakuwa mbali.

Mwenyekiti wa kamati ya jamii  kutoka Tinde Juma Warioba amesema  mbinu hiyo walifundishwa na mashirika mbalimbali ambayo yamekuwa yakileta miradi ya kupinga ukatili kwa wanawake na watoto.

Warioba amesema wanaume walikuwa na tabia ya kudanganya wake zao  msimu wa mavuno kuwa wapeleke mazao kwenye godauni kuhifadhiwa kumbe ndiyo tiketi ya kwenda kuuza bila kushirikisha familia.

“Shirika la Care International,Save the Children,Red cross na WEADO yote yamekuwa yakifanya kazi ya kutoa elimu na kupinga ukatili kwenye kata ya Tinde nab ado yanaendelea ”amesema Warioba.

Ofisa mtendaji  wa kijiji hicho Rukia  Hussein amesema  wanafunzi waliofaulu mwaka huu   kwenye shule ya kijiji hicho   ni 19 ikiwa wasichana nane na wavulana 11.

“Kutokana na mnada wa mifugo kuwa karibu wametumia fursa ya kuhifadhi mifugo badala ya fedha”amesema Hussein.

Mtendaji wa kata hiyo Latifa Mwendapole amesema hakuna tukio lolote lililotokea la ukatili kwa mwaka huu  mashirika yamefanya kazi kubwa wanafunzi wamejitambua  kupaza sauti kwa wazazi wao na kuripoti shuleni vitendo vya kikatili.

Ofisa maendeleo ya jamii  kata ya Tinde  Eva  Mlowe amesema kesi za vitendo vya ukatili  ndani ya familia zilikuwa zaidi kipindi cha mavuno  lakini sasa zimeenda zikipungua.

Shirika la  Woman Eldery Advocacy Development Organization (WEADO)  limeeleza kushiriki kuunda mabaraza ya watoto kwenye  kata za Tinde na Masengwa   ambapo wamejengewa uwezo  masuala ya  haki za mtoto,ukatili dhidi ya mtoto na uongozi wa kishujaa.

 

 

Post a Comment

0 Comments