Header Ads Widget

RPC SHINYANGA AWATAKA WANANCHI KUACHANA NA RAMLI CHONGANISHI ZINAZOSABABISHA MAUAJI KATIKAJAMII

Suzy Luhende, Shinyanga Blog

 

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi amewataka wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuachana na ramli chonganishi ambazo zimekuwa zikisababisha mauwaji ya kujichukulia sheria mkononi.


Agizo hilo amelitoa jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Dome kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga, ulioandaliwa na mwenyekiti wa mtaa wa Dome Solomon Najulwa.


Kamanda Magomi amesema imani za ramli zimekuwa zikichonganisha watu wengi na kusababisha watu kukatana panga na kusababisha vifo, hivyo inatakiwa kupiga vita na kizikwepa imani za ramli kwa sababu zinaleta mauwaji kwa kusingiziana.


"Tabia hizi sio nzuri, hivyo tunatakiwa kukemea na kuachana kabisa na ramli chonganishi, pia tuache kujichukulia sheria mikononi pale anapobainika mtu kaiba kuku, kaiba kitu chochote, kwa sababu sasa hivi huko halmashauri ya Shinyanga mtu akiiba kuku tu anauwawa, hivyo tuache kufanya ukatili wa namna hiyo"amesema Magomi.


Pia amesema kumekuwa na mauwaji yanayosababishwa na watu kugombania mashamba na wivu wa mapenzi huko wilaya ya Kahama na Shinyanga ambapo hivi karibuni kata ya Tinde wilayani Shinyanga mwanamke amemkata panga mme wake baada ya kuona anatoka nje ya ndoa.


"Ugomvi wa namna hii unasababisha watoto kukosa sehemu za kwenda na kusababisha kukimbilia mitaani na kuwa watoto wa mitaani, tuache kugombana tufike mahali tuwe na malezi bora kwa watoto wetu na tuwakemee wasijifunze wizi mdogo mdogo,"amesema Kamanda Magomi.


"Pia kuna baadhi ya watu tunaoishi nao kwenye mitaa yetu wanauza milungi, wanauza bangi lakini hamtoi taarifa, hivyo ili kuweza kulinda watoto wajukuu wetu wasiharibike tunaomba mtupe taarifa ili tushughulike na watu hawa wanaojihusisha na biashara hizo,"ameongeza Magomi.


Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Dome Solomon Najulwa amesema analishukuru jeshi la polisi kwa kuanzisha polisi kata, kwani inawasaidia sana kulinda usalama wa watu na mali zao tangu ianzishwe polisi kata wizi katika mtaa wa Dome umepungua wanaushirikiano mzuri na polisi kata, kwani kila kinapotokea jambo polisi anapatikana kwa urahisi.


Pia baadhi ya wananchi wa mtaa wa Dome Cosmas Edward na Adelta Maleo wamemshukuru kamanda wa jeshi la polisi kwa kuwatembelea katika mtaa wao, wamesema ameonyesha anawajali na kuwapenda kwa sababu amefika mwenyewe kusikiliza kero zao.
Kina mama wa mtaa wa Dome kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga wakitoa zawadi ya kitenge kwa kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga akifurahia zawadi aliyopewa ma akinamama wa mtaa wa Dome

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi akizungumza kwenye mkutano wa mtaa wa Dome

Askari polisi ambaye pia ni msanii wa nyimbo anayejulikana jina la usanii Nyumbu mjanja akiimba kwenye mkutano wa mtaa wa Ndembezi

Viongozi mbalimbali wa chama cha mapinduzi wakiwa kwenye mkutano huo

Wasanii wa sarakasi wanaoishi mtaa wa Dome wakitoa burudani kwenye mkutano wa mtaa wa Dome

Mwenyekiti wa mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Solomon Najulwa akizungumza kwenye mkutano

Katibu mwenezi wa kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga akizungumza

Michael Chacha akitafasiri lugha za alama kwa watu wenye ulemavu wa kutosikia (Viziwi)


Mtendaji wa mtaa wa Dome akisoma taarifa ya mtaa kwenye mkutano huo


Wananchi mbalimbali wa mtaa wa Dome wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya mtaa wa Dome


Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga akipokea zawadi aliyopewa na kina mama wa mtaa wa Dome

Post a Comment

0 Comments