Header Ads Widget

MADIWANI MEATU WASIKITISHWA NA UAMZI WA KUBADILISHWA KWA MPANGO WA BAJETI BILA KUPATA KIBALI CHA BARAZA LA MADIWANI


Mwenyekiti wa halmashauri ya  Meatu Athony Athumani akizungumza kwenye baraza la madiwani
 
Suzy Luhende, Shinyanga blog

BAADHI ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Meatu mkoani Simiyu wamesikitishwa na uamuzi uliofanywa na Menejimenti ya halmashauri hiyo kuchukua maamuzi ya kubadilisha Mpango wa bajeti bila kupata kibali cha Baraza la Madiwani.

Madiwani hao wamesema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria na kanuni za Halmashauri kwa vile Mpango wa Bajeti ulipitishwa rasmi na Baraza la Madiwani kama Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Namba 9 ya mwaka 1982 kifungu cha 43 (i) inavyoelekeza.

Hoja hiyo imeibuliwa na diwani wa Kata ya Mbugayabanya, Masumbuko Pesa ambapo ameelezea kushitushwa kwake na kitendo kilichofanywa na Menejimenti kuhamisha baadhi ya fedha za miradi iliyopitishwa kwenye bajeti na kuzielekeza kwenye miradi ambayo haina Baraka za Baraza la madiwani.

“Mnamo Februari 08, mwaka huu Baraza letu la madiwani lilifanya kikao maalumu kwa ajili ya kupitia na kupitisha Bajeti ya Halmashauri tukizingatia sheria za fedha za Serikali za Mitaa,”

“Lakini hata hivyo katika vikao vya Kamati za Kudumu za Halmashauri ya wilaya vya robo ya kwanza, imeonekana kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni katika utekelezaji wa bajeti ambapo imeonekana miradi mingi iliyopitishwa na baraza haijapangiwa fedha,” ameeleza Pesa.

Ameendelea kufafanua kuwa jambo la kusikitisha ni kuona miradi mipya ambayo haikupitishwa wala kupangwa kupatiwa fedha ndiyo hivi sasa imepangwa kupatiwa fedha jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Diwani huyo ametoa mfano wa baadhi ya miradi ambayo ilipitishwa  na Baraza la Madiwani ili ipatiwe fedha kuwa ni pamoja na mradi wa lishe kiasi cha sh 109,000,000.00 na fedha za kilimo na Ushirika kutokana na Mapato ya ndani sh 50,000,000.00 jumla ikiwa sh 159,000,000.00.

Ameendelea kueleza kuwa fedha zilipangwa ili ziende kukamilisha shughuli za ujenzi wa miundombinu katika Zahanati 10 na zifunguliwe ziweze kutoa huduma kwa wananchi hata hivyo pamoja na kupitishwa kwenye Baraza la Bajeti, zimeondolewa kwenye bajeti.

“Pia katika kupitisha Bajeti ya mwaka 2022/2023 Baraza la Madiwani lilipitisha kiasi cha sh 500,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Afya cha Iramba ndogo na Mwasengela yaani kila Kituo cha afya kilipangiwa kiasi cha sh 250,000,000.00,”

“Hata hivyo fedha hizi hazikuingizwa katika bajeti na badala yake zimebadilishiwa matumizi bila idhini ya Baraza la madiwani na katika hali ya kushangaza Menejimenti imeamua kuzipangia maeneo mengine kinyume na ilivyopitishwa na  Baraza la Madiwani,” ameeleza diwani Pesa.

Pia diwani huyo amehoji kitendo cha mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Masalinge (Lingeka) ambayo imepangiwa kiasi cha sh milioni 600 zilizotolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine ikiwemo maabara.

Amesema katika hali ya kushangaza bado Menejimenti imeamua kutenga fedha nyingine kiasi kingine cha shilingi milioni 73 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya maabara ambavyo tayari vimetengewa fedha kutoka Serikali Kuu hali ambayo anahisi ni upigaji wa fedha za halmashauri.

Kutokana na hali hiyo diwani huyo ameomba yafanyike marekebisho kwenye bajeti yote ya Halmashauri na kuwezesha miradi ambayo awali ilipangwa kupatiwa fedha iweze kupatiwa fedha kama ilivyopitishwa na kwamba ni vyema Menejimenti ikaheshimu mpango wa bajeti uliopitishwa na madiwani.

Kwa upande wake diwani Emanuel Maliganya wa kata ya Sakasaka amesema kuhamishwa kwa bajeti ya halmashauri kimya kimya si utaratibu ndio maana kuna kikao cha baraza la madiwani wanaoketi kupitisha bajeti kwa mujibu wa sheria kila mwaka.

Maliganya amesema ni vyema watendaji wa Halmashauri (Menejimenti) wanakubaliana wajisahihishe na kitendo hiki kisiendelee kujirudia huku akiziomba mamlaka zinazosimamia bajeti za halmashauri zisimamie ipasavyo.

Naye diwani wa kata ya Lubita, Juma Mpina amesema suala la kubadilishwa kwa bajeti wamelipinga kwa asilimia 100, kwa sababu mkurugenzi hayuko sahihi hawezi kuidhinisha fedha bila baraza la madiwani kujua, kufanya hivyo ni kuvunja sheria.

Hata hivyo Mpina  amempongeza  Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akishauri fedha hizo  zinapotoka basi pawepo na utaratibu wa wao madiwani kuoneshwa BOQ za miradi husika ili waweze kusimamia kikamilifu kwa mujibu wa BOQ zinavyoonesha.

“Suala la kubadilishiwa bajeti tumelipinga kwa asilimia 100 huwezi kuchukua fedha bila idhini ya baraza kama wangetaka kubadilisha wangeitisha kikao cha baraza ndipo yakawepo makubaliano, lakini kubadilishwa kinyemela sisi hatukuridhika kabisa, ombi langu   Serikali ilishughulikie jambo hili ili lisijirudie," ameeleza Mpina.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu  Anthony Athumani pamoja na kumtaka diwani wa kata ya Mbugayabanya kuwasilisha andiko lake lenye mapendekezo ya utekelezaji wa bajeti kwenye Kamati ya Fedha ili liweze kufanyiwa kazi na kwamba atafanyia kazi mapendekezo yote na ushauri walioutoa kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Meatu.

Hata hivyo alisema baadhi ya miradi inayodaiwa kutopatiwa fedha mpaka hivi sasa hali hiyo imesababishwa kwa kiasi kikubwa na kuchelewa kupokea fedha kutoka kwa wafadhili kama walivyokuwa wameaahidi na hivyo kulazimika kufanyia marekebisho baadhi ya miradi na ni kwa nia njema.

Akijibu hoja hiyo mkurugenzi wa halmashauri ya Meatu Msoleni Dakawa alisema hoja ya madiwani ni nzuri ila alishauri kuwa mtoa hoja pamoja na madiwani wengine  wakakae na WDC yao wakubaliane ni miradi gani inatakiwa kutekelezwa katika maeneo yao ili hoja hiyo ipelekwe kwenye menejimenti, ambapo atakaa  mwenyekiti afisa mipango na mkurugenzi.


Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi uchumi na hifadhi ya mazingira Mlangale Sakumi


Diwani viti maalumu Pendo Masatu akizungumza kwenye baraza la madiwani


Mwenyekiti wa halmashauri ya  Meatu Athony Athumani akizungumza kwenye baraza la madiwani

Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Meatu Njile Ng"wakwa diwani kata ya Mwabuma 
Mwenyekiti wa halmashauri ya Meatu  Antony Athumani akizungumza kwenye baraza 

Madiwani wa halmashauri ya Meatu wakimsikiza mwenyekiti akifafanua jambo Diwani wa Kata ya Mbugayabanya, Masumbuko Pesa akizungumza kwenye kikao cha baraza la baraza la madiwani 


Mkurugenzi wa halmashauri ya Meatu akifafanua jambo kwenye kikao cha baraza la madiwaniPost a Comment

0 Comments