Header Ads Widget

MKUU WA WILAYA KAHAMA AAGIZA KITUO CHA AFYA KUANZA KUFANYA KAZI KUOKOA VIFO VYA WAJAWAZITO NA WATOTO.
Mkuu wa wilaya ya Kahama  mkoani Shinyanga Festo Kiswaga akikagua jengo la kituo cha afya  katika kata ya Igwamanoni halmashauri ya Ushetu kilichojengwa kwa fedha za tozo.

Na Kareny Masasy, KAHAMA

MKUU wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Festo Kiswaga ameagiza kuanza kufanya kazi mara moja kwa kituo cha afya Igwamanoni kilichopo halmashauri ya Ushetu baada ya kukamilika.

Kituo hicho kilichojengwa kwa fedha za tozo za miamala kwa gharama ya sh Millioni 500 ambapo kata hiyo ilikuwa haina kituo cha afya bali ilikuwa na Zahanati pekee.

Mkuu wa wilaya Kiswaga ameyasema hayo jana alipotembelea kituo cha afya Igwamanoni ambacho kimekamilika kwa asilimia 100 na kujengwa kwa mafundi wazawa (Local fundi)

Ofisa mipango wa halmashauri ya Ushetu Theresia Nsumba alisema kuwa mpaka sasa kuna vituo vya afya vitatu ambavyo ni ukune,Ushetu na Bulungwa na viliwili vimejengwa Nyalwewe na Igwamanoni bado havijaanza kufanya kazi.

“Majengo yaliyojengwa kwenye vituo hivyo vipya ni wodi ya mama na mtoto,jengo la upasuaji,jengo la kufulia,jengo la kuhifadhi taka na jengo la wagonjwa wa nje (OPD)”amesema Nsumba

Nsumba amesema kuwa kuna sh Millioni 300 zilizotengwa kwaajili ya kuendeshea vituo vya afya na utekelezaji wa kuanza kazi kituo cha afya Igwamanoni atakaa na wataalamu wa afya ili kujua vifaa vipi vinahitajika nakuanza kazi kama ilivyoelezwa na mkuu wa wilaya.

Nsumba amesema kuwa halmashauri ya Ushetu ina kata 20,vijiji 112 na Zahanati 27 pia kuna vituo vya afya vitatu tu ambavyo mpaka sasa vinafanya kazi.

Muuguzi wa Zahanati ya kijiji cha Igwamanoni Anasia Nyakeza amesema kuwa kwa mwezi wanaokuja kujifungua kwenye zahanati ni wajawazito 45 hadi 50 na wanahudhuria kliniki ni 60 hadi 65

“Wajawazito wanaokuja kujifungua nakupatiwa rufaa ni wale wanaotokwa na damu nyingi au mtoto kukaa vibaya sasa utakuta hospitali za rufaa ziko mbali na kituo hiki cha afya kitakuwa msaada mkubwa kina mama kupata huduma karibu”amesema Nyakeza.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Igwamanoni Mhoja Magazi na Shija Lubude wamesema kuwa wamefura fedha za tozo kwani zimewaletea maendeleo kwani huduma zilizohitaji rufaa walikuwa wakienda Masumbwe wilaya ya Mbogwe .

"Tumekuwa tukitumia gharama kubwa kwenye usafiri peke yake wakati mwingine tunaambiwa kusafirisha mjamzito anayeumwa uchungu sh 10,000 hadi 15,000 kwa pikipiki au kutembea kwa miguu umbali wa kilomita 28 au kwenda manispaa ya Kahama kilomita 50"amesema Magazi .

Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Doa Limbu amesema kuwa halmashauri hiyo wakazi wake wanaopata huduma karibu za afya ni asilimia 30 na wanaozipata mbali ni asilimia 70

Sera ya afya ya mwaka 2007 inaeleza kuwa kila kata kuwe na kituo cha afya na kila kijiji kuwe Zahanati hivyo serikali inampango mkakati wa kuhakikisha sera hiyo inafanikiwa.

Dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 ina malengo ya kupunguza vifo vya watoto wachanga na vifo vya uzazi kwa robo tatu ya viwango vya sasa na upatikanaji wa huduma za msingi kwa watu wote.

Post a Comment

0 Comments