Header Ads Widget

MGODI WA MWADUI KUANZA KUTOA SH BILION 1.2 KUTEKELEZA SHUGHULI ZA KIJAMII

                  Viongozi wa Halmashauri ya Kishapu wakisaini mkataba wa makubaliano na uongozi wa Mgodi wa Williamson Diamond kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kijamii katika Kata tano zinazozunguka mgodi,aliyesimama katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akishuhudia utiaji wa saini akiwa pamoja na baadhi ya madiwani kutoka Kata zinazozunguka Mgodi pamoja na viongozi wengine. 

 Na Suzy Luhende,Shinyanga Press Club Blog 

Hatimaye wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga wameanza kunufaika na mgodi wa Almasi wa Williamson  Diamond (WDL) kwa kuanza kulipwa sh 1.2 bilioni sawa na asilimia 0.7 ambapo tangu kuanzishwa kwake miaka zaidi ya 80 iliyopita hawakuweza kunufaika na mgodi huo.

 Hayo yameelezwa  kwenye hafla ya kusaini mkataba kati ya halmashauri ya Kishapu na mgodi wa almas Mwadui,  katika ukumbi wa halmashauri hiyo ambapo wamesema toka mgodi huo uanzishwe wananchi walikuwa  wananufaika kidogo na mgodi huo. 

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo mkurugenzi wa halmashauri ya Kishapu Emmanuel Jonson amesema mwaka  2019 /2020 kulikuwa na changamoto kwenye mgodi huo na kusitisha uzalisha lakini mwaka  2021/2022  mgodi ulikuwa ukitoa Sh milioni 156  ambazo utekelezaji wake haukufanyika kwa sababu uzalishaji wake ulianza mwezi wa 11. 

"Mabadiliko haya yataleta maendeleo kwa wananchi kwani fedha hizi zitanufaisha kata tano na vijiji 19  vinavyozunguka mgodi na kutakuwa na  miradi ya aina tatu kuanzia ngazi ya vijiji,Kata na miradi itakayosimamiwa na Wilaya ili kuwaondolea changamoto wananchi”amesema Mkurugenzi Jonson. 

 Amesema kupitia majadiliano waliyofanya na uongozi wa mgodi yamezaa matunda baada ya kusaini mkataba wa Sh bilioni 1.2 sawa na asilimia 0.7  fedha ambayo itakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo kwa Kata zinazozunguka mgodi ili ziweze kunufaika. 

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude amesema jukumu lake  ni kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, hivyo amemtaka meneja wa mgodi huo makubaliano hayo wayatekeleze kwa wakati ,huku akitoa maagizo kwa madiwani wa Kata tano zinazozunguka mgodi kwenda kusimamia miradi itakayotekelezwa kwenye maeneo yao. 

"Miradi hii itekelezwe kwa uaminifu na ikaonekane kwenye jamii, mkurugenzi na wakuu wa idara simamieni vizuri ili miradi hiyo iwe ya kiwango,  na miradi ya kimkakati mliyonayo nawaomba ikaonekane kwa wananchi  ili waweze kunufaika kwa muda mrefu"amesema Mkude. 

Meneja mahusiano ya jamii kutoka mgodi wa Williamson Diamond  Bernard Mihayo,amesema fedha hizo zikatumike kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kutekeleza miradi ya kijamii ambayo iliibuliwa na wananchi na si kwa matumizi mengine ambayo hayakupangwa. 

Mwanasheria  wa mgodi huo Sylvia Leonidas amesema  mkataba huo ni baina ya Williamson na halmashauri ya Kishapu na wametengeneza mkataba kwa kuzingatia misingi ya kisheria ya sheria ya  madini ya mwaka 2010 toleo la 2019 kipengele cha 105  ambacho kilifanyiwa marekebisho mwaka 2017.Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mgodi wa Williamson Diamond ambaye pia ni Meneja mahusiano na jamii Bernard Mihayo akizungumza baada ya kusaini mkataba wa makubaliano na Halmashauri ya Kishapu.

               Zoezi la kusaini mkataba likiendelea
                                           Viongozi wakisaini mkataba

                                          
 

Post a Comment

0 Comments