Header Ads Widget

MANISPAA SHINYANGA KUWAINUA KIUCHUMI WANANCHI KUPITIA FEDHA ZA MAPATO YA NDANI

 
 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura (katikati) akionesha sehemu ya mipapai ambayo imepandwa na moja ya vikundi vya wanawake waliopewa mkopo kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo katika eneo lililoandaliwa na Manispaa ya Shinyanga.

Na Suleiman Abeid, SHINYANGA

HALMASHAURI ya Manispaa ya Shinyanga imetenga zaidi ya shilingi milioni 450 zinazotokana na makusanyo yake ya ndani kwa ajili ya kuwakwamua kiuchumi wananchi wake.

Mkurungenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura amesema kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya mapato yake ya ndani kitakachotumika katika kutengeneza eneo maalumu litakalotumiwa na vikundi vya vijana na wanawake kuendeshea shughuli zao mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Satura amesema mbali ya kiasi hicho cha fedha pia Manispaa imetenga eneo la zaidi ya ekari 30 kwa ajili ya kuendeshea shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga.

Amesema anaamini maeneo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa wakazi wa Manispaa ya Shinyanga watakaokuwa tayari kujitokeza kufanya shughuli za uzalishaji mali upande wa sekta ya viwanda vidogovidogo na ujasiriamali.

Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa kutokana na Manispaa ya Shinyanga kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 na kuongonza Kitaifa upande wa Manispaa nchini wakiwa wamevuka lengo la makusanyo kwa asilimia 120 wameamua sehemu kubwa ya mapato hayo kuyarejesha kwa jamii yenyewe.

Kuhusu eneo lililotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo amesema tayari vipo vikundi vya vijana na wanawake vimeanza kuendesha shughuli za uzalishaji kwa kulima mazao ya chakula na mbogamboga na kwamba Manispaa imetengeneza miundombinu yote muhimu kwenye eneo hilo ikiwemo kuweka maji ambayo yatawawezesha wahusika kulima pasipo kutegemea mvua.

“Kwa hivi sasa tumeanzisha utaratibu mpya katika utoaji wa mikopo hii inayotokana na asilimia 10 ya mapato yetu ya ndani, kila kikundi kinachokuja kuomba mkopo lazima katika andiko lake kioneshe jamii ya Shinyanga itanufaika vipi na shughuli watakazozalisha,”

“Tayari tuna eneo la shughuli za kilimo kule Lubaga, tuna zaidi ya ekari 30 na tayari kuna vikundi vya vijana na wanawake vimeanza uzalishaji katika eneo hilo, matunda ya shughuli zao tumeanza kuyaona baada ya bei ya matunda ikiwemo papai na hata mchicha kupungua katika mji wetu,” anaeleza Satura.

Kwa upande wa vikundi vya wanawake, anasema ofisi yake imenunua jengo ambalo tayari lina mashine za kisasa za kukobolea na kusaga nafaka ambalo litatumiwa na vikundi vitakavyokuwa vimepatiwa mkopo kutoka mfuko wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

“Kama nilivyosema hapo awali, jengo hili lina mitambo yote muhimu ya kuendeshea shughuli za ukoboaji na usagaji wa nafaka na tumejenga jengo lingine kwa nje yake litakalotumika kwa ajili ya kuuzia mchele na unga, na nyuma ya jengo hilo kuna mabwawa matatu yatakayotumika kwa ufugaji wa samaki,”

"Lakini mbali ya shughuli hizo za uzalishaji mali, Manispaa yetu imepelekea kiasi cha shilingi milioni 112.5 katika shule ya msingi Bugweto kwa ajili ya ujenzi wa vyumba sita vya madarasa na ofisi mbili za walimu baada ya majengo mengi ya shule hiyo kuchakaa, na kwamba pia fedha hizo zimetokana na mapato ya ndani," anaeleza Satura.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wamempongeza Mkurugenzi wa Manispaa yao kwa ubunifu mkubwa anaoufanya ambapo wamesema mikakati aliyoianzisha itainua kwa kiasi kikubwa kipato cha wakazi wa Shinyanga na kukuza uchumi wao.

Mmoja wa wakazi hao amewambia waandishi wa habari kwamba ubunifu wa kuvipatia vikundi vya vijana na wanawake mikopo kwa utaratibu ambao umeanzishwa na Mkurugenzi utaviwezesha vikundi vinavyokopeshwa mikopo hiyo kurejesha kwa wakati pasipo tatizo.

“Sijapata kuona Mkurugenzi mbunifu kama huyu, haya mambo anayoyafanya ni makubwa, nimeona kule Lubaga lile eneo sasa watu wataweza kulima mazao mbalimbali kwa mwaka mzima pasipo kutegemea mvua za masika, maana amewawekea miundombinu ya maji yanayopatikana wakati wote,”

“Kwa hali hii ni wazi vikundi vitakavyopatiwa mkopo kwa ajili ya kuendeshea shughuli za kilimo havitashindwa kurejesha kwa wakati mkopo waliokopeshwa, maana eneo hilo halina hofu ya ukame, maji ya uhakika yanapatikana wakati wote,” anaeleza Samwel Maganga.

Kwa upande wao wakazi wa eneo la Bugweto wamemshukuru Mkurugenzi Satura kwa kuipatia shule yao ya msingi ya Bugweto kiasi cha shilingi milioni 112.5 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba sita vya madarasa hali itakayowawezesha watoto wao kusoma kwenye majengo mazuri baada ya yale ya zamani kuchakaa.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugweto, Agnes Stansilaus anasema kwa kipindi kirefu shule yake ilikuwa ikikabiliwa na uchakavu mkubwa wa vyumba vya madarasa pamoja uhaba wa vyoo kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na walimu.

Mwalimu Agnes anasema baada ya kumweleza mkurugenzi hali halisi ilivyo katika shule hiyo aliitembelea na kujionea hali halisi ilivyo ambavyo hata yeye alionesha kusikitishwa na hivyo kuahidi kusaidia katika kutatua changamoto hiyo kwa kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kujenga vyumba sita vya madarasa na ofisi mbili za walimu. 
 
“Kwa kweli miundombinu ya shule yetu hapo awali ilikuwa ni mibovu sana hasa upande wa vyumba vya madarasa, vingi vimechakaa kutokana na mazingira ya eneo letu kuwa la mbuga, lakini baada ya mkurugenzi kututembelea alijionea hali halisi, na akatupatia kiasi cha shilingi milioni 112.5 kwa ajili ya ujenzi vya vyumba sita na ofisi mbili za walimu,” anaeleza Agnes.

Agnes anaendelea kueleza kuwa kitendo cha Mkurugenzi kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba sita vya madarasa kimepongezwa pia na wananchi wa Bugweto ambao na wao wamejitolea kumuunga mkono Mkurugenzi wao kujenga vyumba viwili vya madarasa ambavyo tayari wameanza kujenga msingi wake.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura (katikati) akionesha sehemu ya mipapai ambayo imepandwa na moja ya vikundi vya wanawake waliopewa mkopo kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo katika eneo lililoandaliwa na Manispaa ya Shinyanga.
Jengo la watumishi katika Zahanati ya Mwamalili ambalo limejengwa na Manispaa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani kwa lengo la kuwawezesha watumishi kuishi jirani na eneo la kazi.
Sehemu ya vyumba sita vya madarasa na ofisi mbili za walimu vinavyojengwa katika shule ya msingi Bugweto kwa fedha za mapato ya ndani.
 
Sehemu ya mashine za kukoboa na kusaga nafaka pamoja na jengo zilizomo mashine hizo ambalo limenunuliwa na Manispaa kwa ajili ya kuvisaidia vikundi vya wanawake vinavyojishughulisha na shughuli za uuzaji wa nafaka mbalimbali ikiwemo unga na mchele.

Post a Comment

0 Comments