Header Ads Widget

MLINZI AUAWA NA WATU WASIOJULIKANA WALIOFIKA KUIBA MCHELE MASHINENI

 NA HALIMA KHOYA, SHINYANGA.

Mlinzi wa Kampuni ya Ndelumo Security Geofrey Justine (45) ameuawa kwa kunyongwa na watu wasiojulikana katika Kata ya Didia wilayani Shinyanga, wakati akiwa kwenye eneo lake la ulinzi katika Mashine ya Bwana Richard Mwagi.


Mwenyekiti wa kijiji cha Didia wilayani Shinyanga Mrisho Hamadi, amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu, kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Septemba 24 mwaka huu.

Amesema kuwa watu hao walimvamia mlinzi huyo kwa kumvizia na kisha kuanza kumshambulia na kumnyonga shingo na kusababisha kifo chake.

"Marehemu tumemkuta na majeraha katika kichwa chake huku akitokwa na damu mdomoni,"amesema Hamadi.

"Katika Mashine ambayo alikuwa akilinda tumekuta kumefanyika wizi wa Kilo 500 za Mchele wenye thamani ya Sh; milioni 1.2,"anaongeza.

Aidha, Marehemu huyo nyumbani kwao ni Karagwe mkoani Kagera na alikwenda kijijini humo kwa ajili ya kutafuta riziki na kupata kazi ya ulinzi katika mashine hiyo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa Shinyanga (RPC) Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Mlinzi huyo alivamiwa na watu wasiofahamika pamoja na kuiba mchele wenye kilo 500 katika mashine hiyo.

“Ni kweli tukio hilo limetokea katika kata ya Didia Tarafa ya Itwangi Wilaya ya Shinyanga Mkoani hapa ambapo watuhumiwa wa tukio hilo tunawatafuta,"amesema Kamanda Magomi.


Post a Comment

0 Comments