Header Ads Widget

UKUAJI WA MTOTO KIAKILI HUTEGEMEA UNYONYESHAJI ULIO BORA.


 UKUAJI WA MTOTO  KIAKILI HUTEGEMEA  UNYONYESHAJI ULIO BORA.

Na  Kareny  Masasy

MAZIWA  ya mama ni maalumu kwa ajili ya lishe ya mtoto, yana virutubishi vyote anavyohitaji na humkinga dhidi ya maambukizi.

Faida za Unyonyeshaji wa maziwa ya mama unawawezesha mamilioni ya watoto wachanga na wadogo kuishi na kuwa na maendeleo mazuri ya ukuaji.

Sheila Mohamood  anasema kuwa   elimu ya unyonyeshaji mtoto baada ya  kuzaliwa aliipata  hospitalini  lakini amekuwa akijitahidi kunyonyesha mtoto wake ipasavyo na sasa ana umri wa mwaka mmoja na nusu.

Pachazia John anasema kuwa  amemuachicha mtoto wake wa mwaka mmoja ili ale na vyakula vingine  anakiri elimu ya unyonyeshaji mpaka miaka miwili ameelezwa na wataalamu wa afya kliniki.

Samson Peter na Musa Onesmo wanasema kuwa mtoto ni haki yake kunyonya  ndiyo maana wataalamu wanawaeleza wanawake wanyonyeshe  miezi sita mfululizo bila kumpa kitu kingine.

Ofisa lishe  halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga  Peter  Shimba anasema kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama unaupatia nguvu mfumo wa ukuaji na maendeleo ya ufahamu na utambuzi (IQ) wa mtoto.

 Shimba anasema kwa  kiasi kikubwa husaidia katika kuimarisha mafanikio ya elimu, ushiriki katika nguvu kazi na kuongeza kipato katika maisha ya baadaye ya mtoto.

“Wapo wazazi ambao wamekuwa wakinga’ang’ania kuwekeza  kwa mtoto umri ambao  ubongo umekwisha komaa hauwezi tena  watoto wote wanazaliwa na akili wajitahidi kwenye unyonyeshaji”anasema Shimba

Ofisa lishe mkoa wa Shinyanga Denis Madeleka anasema kuwa kwa mkoa wa Shinyanga  una asilimia 83 ya watoto wanaonyonya maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita pekee.

Madeleka anasema kuwa  watoto wenye umri wa miezi 0 hadi 23  ni asilimia 99 walioanzishiwa  maziwa ya mama ndani ya saa moja na walioendelea kunyonya  baada ya saa moja  ni asilimia 3.9.

 “Waliondelea kunyonya baada ya mwaka mmoja ni asilimia 78 wazazi wanaelezwa  umuhimu wa kunyonyesha watoto baada ya kuazaliwa na baada ya kufikisha umri wa  mwaka mmoja  ikiwa wataalamu kwenye  vituo vya afya wameendelea kutoa elimu”anasema  Madeleka.

Kwa mujibu wa Taasisi ya chakula na lishe  nchini( TFNC )  inaeleza mnamo mwaka 1990  mkutano wa wataalamu wa lishe ulifanyika  nchini Italia  lengo  kujadili mwelekeo wa kisera kuhusu kuendeleza unyonyeshaji Watoto maziwa ya mama.

Mkutano huo uliohisaniwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya WHO (Shirika la Afya Duniani) na UNICEF (Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto) Ulifanyika  mwaka 1990

Azimio lililopitishwa na nchi wanachama  kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kuweza kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo .

Pia azimio hilo limewataka wanawake kunyonyesha baada ya kujifungua na kuendelea kuwanyonyesha watoto wao hadi watimize umri wa miaka miwili au zaidi.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mwanaidi Khamis wakati akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu  anasema asilimia 97 ya watoto wanaozaliwa hunyonyeshwa maziwa ya mama.

Naibu waziri Khamis  anasema pia asilimia 92 ya watoto hunyonyeshwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na kuendelea.

Naibu waziri Khamis  anasema  kuwa 43% ya watoto  ndio hunyonyeshwa hadi kipindi cha miaka miwili na kuendelea .

Naibu waziri Khamis anasema kuwa  takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 57  ya watoto ndiyo hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kuchanganya na chakula kingine ndani ya kipindi cha miezi 6.

"Tafiti zinaeleza kuwa mtoto akizaliwa na kuanza kunyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa moja kunaweza kuokoa uhai wake kwani kuchelewa kumnyonyesha mtoto kuna changia kwa kiwango kikubwa vifo vya watoto wachanga ndani ya siku 28." anasema Khamis .

Naibu Waziri huyo aliwahimiza wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoa huduma kwa wakati husika na kuwaasa wazazi kuendelea kuhudhuria Kliniki kama inavyoagizwa

"Kunyonyesha maziwa ya mama kuna faida nyingi kwa mama na mtoto kwa kuwa kunaimarisha afya na ustawi wa mama na mtoto, huzuia aina zote za utapiamlo  kwa mtoto kwa vile kuna kuwa na uhakika wa chakula"anasema Khamis

Naibu waziri Khamis anasema serikali itaendelea kuimarisha na kuendeleza juhudi za kulinda Afya ya watoto kupitia unyonyeshaji maziwa ya mama,  kutenga fedha na kufuatilia utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo .

Naibu waziri Khamisi anasema faida nyingine  ya   unyonyeshaji ni kuwajengea afya njema ambayo itawafanya wawe wenye mafanikio katika maisha yao nani  chanzo bora cha virutubishi na kinga ya mwili.

 

Post a Comment

0 Comments