Header Ads Widget

TIC YAPOKEA UJUMBE KUTOKA JUMUIYA YA NCHI ZA KIARABU

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimepokea ujumbe kutoka Jumuiya ya nchi za Kiarabu Julai 19, 2022 katika ofisi zake zilizopo mtaa wa Shaban Robert jijini Dar es Salaam.

Ujumbe huu umefanya ziara ya kikazi nchini Tanzania tangu tarehe 17 Julai 2022 na lengo la ziara yao ni kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo na mifugo ikiwa ni msingi wa kuhakikisha usalama wa chakula kwa nchi za kiarabu ambazo mazingira yake ni ya jangwa.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe(Mb) amewakaribisha wawekezaji hao na kuwaambia kuwa Tanzania na Oman ni washirika wa muda mrefu hasa katika fursa mbalimbali za kibiashara.

“Hata hivyo, hatujatumia fursa hizo kikamilifu, ninaamini tunaweza kufanya vizuri zaidi kwa sasa na ninatoa wito kwa mamlaka za serikali katika nchi zote mbili kufanya kazi kwa pamoja ili kuruhusu mtiririko mzuri wa bidhaa na huduma kati ya nchi hizi mbili” alisema Kigahe.


Mhe. Kigahe amesema ujumbe huu unaangazia mnyororo wa thamani wa Kilimo na Mifugo kwa madhumuni ya kutatua usalama wa chakula duniani na kwamba Tanzania inaungana na kuwa nchi yenye nguvu ya kilimo barani Afrika na miradi hii itaongeza kasi ya safari kuelekea mafanikio hayo.


“Hadi kufikia Juni, 2022 jumla ya Miradi 62 ya Uwekezaji imesajiliwa nchini Tanzania na raia wa Oman, miradi hii inatarajiwa kutoa ajira 2,488 ikiwa na thamani ya Uwekezaji wa zaidi ya Dola za Marekani Milioni 308.35 na sekta zinazoongoza katika idadi ya miradi ni viwanda na majengo ya biashara, uchukuzi na utalii na sekta zote hizi zinachangia zaidi pato la Taifa”, aliongeza Mhe. Kigahe.


Naye balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah A. Kilima aliyeambatana na ujumbe huu amesema, ziara hii ni hatua za utekelezaji wa maombi yaliyojitokeza wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alipotembelea nchini Oman mwezi Juni, 2022.


“Ujumbe huu umejumuisha wawakilishi kutoka taasisi za Oman Food Investment Holding Company ambao ndio waratibu wakubwa wa ziara hii na muwakilishi wake ni Mhandisi Saleh Al Shanfari ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu. Lakini pia ziara hii imejumuisha taasisi ya Arab Authority for Agriculture Investment and Agriculture Development ambayo imewakilishwa na Mhe. Mohammed Mazrooei, Mwenyekiti na Rais wa Mamlaka husika ambaye pia ndie kiongozi wa ujumbe huu” alisema Mhe. Kilima

Taasisi nyingine zilizoambatana na ujumbe huu ni pamoja na Arab Bank for Economic Development in Africa ambayo imewakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wake Mhe. Dkt. Sidi Ould Tah pamoja na kampuni ya Al-Rajhi International for Investment kutoka Saudi Arabia.

Ujumbe huu pia umehusisha wawakilishi kutoka Mamlaka ya Uwekezaji nchini Oman (Oman Investment Authority-OIA) pamoja na kampuni ya nyama ya Al-Bashayer Meat Co. SAOC.


Kaimu Mkurugenzi Uhamasishaji Uwekezaji wa TIC ndugu Revocatus Rasheli amesema, hivi sasa tumepata wawekezaji ambao wamefika ambao wamejikita katika eneo la kilimo na ufugaji na hii ni kwenye eneo lote la usalama wa chakula ambapo sisi kama nchi ndio maeneo ya kipaumbele katika mpango wetu wa miaka 5.


“Katika majadiliano yanayoendelea TiC imeratibu na imeweza kuwaleta wadau mbalimbali wa taasisi za serikali na binafsi zinazohusika na uwekezaji na biashara katika sekta hizo za kilimo na uzalishaji wa mazao ya biashara pamoja na mifugo”, alisema Rasheli.


Ujumbe huu pia umetembelea na kukutana na Ranchi ya Taifa NARCO, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), SUMA JKT, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, pamoja na Bodi ya nyama.

Post a Comment

0 Comments