Header Ads Widget

DC KISHAPU AWATAKA WANANCHI KUWEKA AKIBA YA CHAKULA KUEPUKA NJAA

                        Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude

Na Shinyanga press Club Blog

 Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude amewatahadharisha wakazi wa Wilaya hiyo kuweka akiba ya chakula badala ya kukimbilia kuuza kiholela,kutokana na mavuno ya msimu huu kuwa machache na kusababisha kuwepo tishio la njaa katika maeneo mengi ya Wilaya hiyo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Kishapu na kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Emmanuel Jonson kupitia idara ya  kilimo kufanya tathimini kila Kijiji na Kata ili kujua kuna upungufu wa kiasi gani wa chakula kwenye kaya na kujua kwa mwaka huu wamevuna kiasi gani.

Mkuu wa Wilaya amesema  kuwa na takwimu sahihi zitasaidia kupata idadi kamili ya akiba ya chakula kilichopo na mahitaji ya kila eneo,hatua ambayo itasaidia kuondoa usumbufu pindi inapotokea changamoto na kuwa rahisi kukabiliana nayo.

“Waelimisheni wananchi kuweka akiba ya chakula na wasikimbilie kuuza kiholela kwani hali ya chakula msimu huu siyo nzuri,mavuno ni machache na ndiyo maana nimemuelekeza Mkurugenzi kupitia idara ya kilimo kufanya tathimini ili tujue kuna upungufu kiasi gani na maeneo yapi yanachangamoto”amesema Mkuu wa Wilaya ya Kishapu.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniface Butondo ameiomba serikali kudhibiti uuzaji wa chakula nje ya nchi ili kupunguza bei ya vitu kuendelea kupanda kwa kasi vikiwemo vyakula ili kuwawezesha wananchi kununua kwa bei ya chini tofauti na sasa bei ilivyo sasa.

Butondo amesema wakulima wengi Kishapu wanalima mtama,uwele,viazi na mahindi lakini kwa msimu wa mwaka huu mavuno yamekuwa machache na maeneo mengine hawakuvuna kutokana na kukauka na jua,huku akiwataka wananchi wanaotumia mtama na mahindi kutengeneza pombe za kienyeji kuchukuwa tahadhari kutokana na kuwepo tishio la njaa.

Katika hatua nyingine amewaomba wananchi kujitokeza kuhesabiwa katika sensa itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu na kuepuka kuwaficha majumbani watoto wenye ulemavu kwani wote wanahaki ili serikali iweze kupanga mipango mizuri ya maendeleo kulingana na idadi ya watu. 

                       Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniface Butondo akiwahamasisha wananchi wa Kishapu kujitokeza kuhesabiwa wakati wa Sensa Agost 23 mwaka huu.
Madiwani wa Halmashauri ya Kishapu wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani.

Kikao cha baraza kinaendelea
Kikao cha baraza kinaendelea

Post a Comment

0 Comments