Header Ads Widget

SIMULIZI YA JANETH INAVYOFUTA DHANA POTOFU MATUMIZI YA NJIA ZA UZAZI WA MPANGO KWA WANAWAKE

Damian Masyenene

WAKATI Serikali na wadau wakipambana kuelimisha jamii na kuongeza uelewa wa matumizi ya njia za uzazi wa mpango na faida zake kwa maendeleo ya watu na taifa, changamoto imebaki kwa baadhi ya wanajamii kuendelea kueneza dhana potofu juu ya matumizi ya njia hizo huku wengine wakienda mbali kwa kuwaogopesha akina mama wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango kuwa watapoteza uwezo wa kuzaa ama watachelewa kupata watoto.

Mara kadhaa Serikali imesisitiza kuwa matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango ni sahihi na salama japo kuna maudhi madogo yanayoweza kumtokea mtu huku wadau wa afya nao wakibainisha kuwa uzazi wa siyo kumpangia mtu idadi ya watoto bali kuwa na watoto unaoweza kuwatunza na kuwahudumia.

Inaelezwa pia kuwa hakuna dini inayopinga uzazi wa mpango isipokuwa njia zinazotumika ambapo wakatoliki wanakubaliana na uzazi wa mpango isipokuwa hawakubaliani na njia za kisasa (wanataka njia za asili) huku waprotestanti na waislamu wakiukubali lakini wanapinga njia ambazo zinahusika kuharibu mimba.

Janeth Mahundi (siyo jina halisi) mwenye umri wa miaka 28, mama wa mtoto mmoja anathibitisha kuwa matumizi ya uzazi wa mpango hayana athari na hayamfanyi mwanamke kukosa uwezo wa kuzalisha, simulizi yake inawatoa hofu akina mama wengi ambao wamekuwa wakipotoshana kwa kukosa elimu sahihi juu ya afya ya uzazi.

Mama huyo mkazi wa jijini Mwanza mwenye mtoto mmoja wa mwaka mmoja na miezi nane ambaye aliyezaliwa Oktoba, 2020, anasema aliamua kutumia uzazi wa mpango ili kuepuka kupata mimba ya karibu kabla mwanae hajakua na yeye mwenyewe hajakomaa na kuwa tayari kubeba ujauzito mwingine.

“Baada ya kujifungua mwaka 2020 mwezi wa 12 niliweka kipandikizi cha muda wa miaka mitatu nilitaka mwanangu afikishe miaka miwili diyo nibebe ujauzito mwingine lakini baadaye nilibadili mawazo baada ya kuona mwanangu amekua amefikisha mwaka mmoja na miezi sita nikamshawishi mme wangu tutoe kipandikizi ili sasa watoto wapishane miaka miwili na tuzae mapema tupumzike,” anasimulia Janeth.

“Ilikuwa ngumu kidogo hakunielewa kwanini imekuwa mapema hivyo lakini tulifikia muafaka mwezi wa tatu mwaka huu nikatoa kipandikizi na baada ya wiki mbili hivi nikabeba ujauzito, tayari ujauzito umekua una miezi mitatu na wiki kadhaa na mwanetu amefikisha mwaka mmoja na miezi nane, Mungu akipenda nitajifungua mwezi wa 12 ama wa kwanza mwanetu akiwa tayari ana miaka miwili na miezi miwili,” anasema na kuongeza

“Kiukweli wakati ule nimeweka kipandikizi nilipata maneno mengi ya kuchanganya tukiwa tunakutana wanawake kwenye shughuli zetu nikawa naambiwa uzazi wa mpango ni mbaya utanifanya nisizae tena eti utaninenepesha na kupeleka uzazi mbele, kwahiyo wamama tumekuwa tukiogopesha labda hatuna elimu sahihi,”

Mshauri wa afya ya uzazi na Malezi, James Mlali anasisitiza kuwa faida za uzazi wa mpango ni kulinda afya ya mama na mtoto, kusaidia wenza kujua muda muafaka wa kupata mtoto, kugeuza nguvukazi iliyopo iweze kuzalisha mali na siyo kuwa tegemezi ambapo uzazi katika umri mdogo ni hatarishi kwa mama na mtoto kwani tumbo la uzazi la mwanamke huwa tayari kubeba mimba akiwa na umri wa miaka 20 na huwa salama na tayari kubeba mimba kila baada ya miaka miwili au mitatu na ni salama kubeba mimba nne.

“Uzazi wa mpango unatusaidia kupunguza kasi ya kuzaliana na ni muhimu ili kuigeuza nguvu kazi iliyopo iweze kuzalisha rasilimali kwani maandiko yanasema asiyeweza kuwatunza wa nyumbani mwake ni mbaya zaidi kuliko asiyeamini na huwezi kuzaa tu bila kujipanga namna ya kulea,”

“Pia hupunguza vifo vya uzazi, vifo vya mama na mtoto, mahusiano ya wanandoa kuimarika, watoto kupata na kuwa na lishe bora, husaidia kulea vyema watoto, kuwa na familia zenye afya, kutoa elimu bora na nafasi za ajira na kupunguza uharibifu wa mazingira,” anasema Mlali.

Serikali kupitia wizara ya afya imeongeza kasi ya upatikanaji dawa za uzazi wa mpango ambapo kuanzia Julai 2021 hadi Machi 2022 ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango dozi 1,755,349 sawa na asilimia 82 ya lengo, sindano za uzazi wa mpango aina ya depo-provera dozi 2,125,625 sawa na asilimia 93 ya lengo na vipandikizi 206,000 sawa na asilimia 78 ya lengo ambapo dawa hizo zilisambazwa katika halmshauri zote nchini.

Post a Comment

0 Comments