Header Ads Widget

WAJAWAZITO WANAOJIFUNGULIA KLINIKI WAONGEZEKA, VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI VYAPUNGUA NCHINI

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu


Na Damian Masyenene

IMEELEZWA kuwa wanawake wenye ujauzito wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini wameongezeka kulinganisha na kipindi cha nyuma huku vifo vitokanavyo na uzazi navyo vikiendelea kupungua kutokana na akina mama hao kuhudhuria kliniki na serikali kuendelea kuimariisha upatikanaji wa huduma za afya wakati wa ujauzito (Antenatal Care).

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu leo Mei 16, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara ya afya kwa mwaka 2022/23 ambapo inakadiriwa kuwa kila mwaka akinamama wapatao milioni 2.3 hutarajiwa kupata ujauzito nchini Tanzania.

Amesema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022 wajawazito 1,398,778 walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya sawa na asilimia 79.5 ikilinganishwa na wajawazito 890,909 sawa na asilimia 80 ya waliojifungulia kliniki kipindi kama hicho mwaka 2020 huku wajawazito 1,340,239 wakihudumiwa na watoa huduma wenye ujuzi ikilinganishwa na wajawazito 851,040 waliohudhuria kliniki kipindi kama hicho mwaka 2020.

Amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu zinazokusanywa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini zinaonesha vifo vitokanavyo na uzazi vimeendelea kupungua kutoka vifo 1,640 mwaka 2020 hadi vifo 1,580 mwaka 2021 ambapo takwimu hizo hazijumuishi vifo vinavyotokea kwenye ngazi ya jamii.

“Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, jumla ya wanawake wajawazito 1,784,809 walihudhuria Kliniki na kupatiwa huduma za afya na kati yao, asilimia 99.7 ya akinamama wajawazito walifanya mahudhurio manne au zaidi ikilinganishwa na asilimia 85 mwaka 2020, hata hivyo changamoto iliyopo ni wanawake wajawazito kuchelewa kuhudhuria klinik wapatapo ujauzito,” amesema Ummy.

“Takwimu zinaonesha kuwa kati ya wajawazito 1,784,809 ni wajawazito 656,040 sawa na asilimia 37.6 walianza kupata huduma za wajawazito chini ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito ikilinganishwa na asilimia 36 ya kipindi kama hiki mwaka 2020,” ameongeza.

Waziri huyo ameeleza kuwa ongezeko hilo la matumizi ya huduma za kliniki wakati wa ujauzito limetokana na kubadilika kwa mwongozo wa huduma muhimu wakati wa ujauzito kutoka mahudhurio ya kila baada ya miezi mitatu na kuwa mahudhurio ya kila mwezi pamoja na kuongezeka kwa uhamasishaji juu uhumimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki ngazi ya jamii.

“Nitumie Bunge lako Tukufu kuhimiza wajawazito kuhudhuria kliniki mapema ndani ya wiki 12 za mwanzo wa ujauzito na kukamilisha mahudhurio yote 8 ili kuepuka kupata changamoto mbalimbali zinazoweza kusababisha vifo vyao na vichanga vyao wakati wa kujifungua,” amesisitiza.

Kuhusu vifo vya watoto, Ummy amesema kulingana na takwimu zinazokusanywa kutoka vituo vya kutolea huduma zinaonesha kuwa vifo hivyo vimeendelea kupungua mwaka hadi mwaka ambapo vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 8,190 mwaka 2020 hadi vifo 6,741 mwaka 2021.

“Vifo vya watoto wa chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka vifo 2,657 mwaka 2020 hadi vifo 1,092 mwaka 2021 na vifo vya watoto umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 3,482 mwaka 2020 hadi vifo 1,512 mwaka 2021, takwimu hizi hazijumuishi vifo vinavyotokea kwenye ngazi ya jamii,” amebainisha Ummy.Post a Comment

0 Comments