Header Ads Widget

TAKUKURU SHINYANGA YABAINI MADUDU MIRADI MINNE YA MAENDELEO, UKIWAMO UJENZI KITUO CHA AFYA SALAWE


Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga Hussein Mussa akizungumza na vyombo vya habari.
Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga Hussein Mussa akizungumza na vyombo vya habari.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga, imebaini kuwapo na dosari kwenye ujenzi wa miradi minne ya maendeleo, kati ya miradi 18 ambayo imeikagua yenye thamani ya Sh.bilioni 13.7.

Mkuu wa Takukuru mkoani Shinyanga Hussein Mussa, amebainisha hayo leo Mei 20, 2022 wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa vyombo vya habari ya Robo tatu ya mwaka wa fedha (2021-2022), kuanzia Januari hadi Marchi mwaka huu.

Amesema kwa kipindi hicho wamefanya uchunguzi kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo 18, ambayo inatekelezwa mkoani humo yenye thamani ya Sh.bilioni 13.7 ambapo kati ya miradi hiyo minne imekutwa na dosari, na kutoa ushauri ifanyiwe marekebisho ili iendane na thamani halisi ya fedha.

“Miradi minne ambayo tumeikuta ina dosari ni ujenzi wa shule ya Sekondari ya wasichana Butengwa msingi wake kujengwa chini ya kiwango, Shule ya Sekondari Usule haikujengwa miundombinu ya wanafunzi wenye ulemavu, na ujenzi wa barabara za Changalawe Manispaa ya Shinyanga kujengwa chini ya kiwango,” amesema Mussa.

“Mradi mwingine ambao tumebaini una mapungufu ni ujenzi wa kituo cha Afya Salawe, umekuwa na dosari kwenye upande wa manunuzi ya vifaa vya ujenzi na uchunguzi wake unaendelea,”ameongeza.

Aidha, amesema katika kipindi hicho Taasisi hiyo pia ilifanya kazi ya uchambuzi wa mfumo katika Manispaa ya Shinyanga kwa wakala wa huduma ya ununuzi Serikalini (GPSA), na wakala wa umeme na ufundi (TAMESA) na kuziba mianya ya Rushwa iliyobainika katika Taasisi hizo.

Katika hatua nyingi amesema katika dawati la uchunguzi wamepokea taarifa 48 za malalamiko, zinazohusu Rushwa ni 35 na nyingi 13 siyo za Rushwa, na kati ya taarifa hizo za Rushwa 35, taarifa 17 uchunguzi wake unaendelea, 13 uchunguzi umekamilika, Tano uchunguzi umefungwa kwa kukosa ushahidi, Nne zimehamishiwa idara nyingine, 9 zilitolewa ushauri.

Ametaja kesi ambazo zinaendelea Mahakamani ni 18, kesi Sita ziliamuliwa na kesi Nne zilishinda na watuhumiwa kutiwa hatiani na kulipa faini, na kutoa wito kwa wananchi wa mkoa huo wa Shinyanga kuendelea kutoa taarifa za Rushwa kwenye Taasisi hiyo.

Post a Comment

0 Comments