Header Ads Widget

KIJANA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI UPANDE WA MOYO NDANI YA MGODI WA ALMASI EL-HILALI WILAYANI KISHAPU

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga George Kyando akizungumza na vyombo vya habari leo.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamsaka mlinzi Chacha Emmanuel wa kampuni ya ulinzi Sam Security, ambaye analinda ndani ya mgodi wa madini ya Almasi El-Hilali uliopo wilayani Kishapu, kwa madai ya kumpiga Risasi kijana Hamis Mayunga (27) upande  wa kushoto wa moyo akiwa ndani ya mgodi huo na kufariki papo hapo.


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga George Kyando, akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Mei 23, 2022 amesema tukio hilo limetokea Mei 20 mwaka huu majira ya saa 4 usiku.

Amesema Marehemu Hamis Mayunga alikuwa na wenzake zaidi ya 10 wakivua Samaki katika bwawa lililopo ndani ya mgodi huo wa El-Hilali, ndipo walinzi hao walipofika na kuwazuia kuvua Samaki, lakini kukatokea kutoelewana na hatimaye kusababisha mauaji.

"Wakati mzozo ukiendelea kwenye bwawa hilo ndipo mlinzi mmoja Emmanuel Chacha akiwa na wenzake Wanne, akamfyatulia Risasi na kumpiga upande wa kushoto wa moyo na kufariki dunia papo hapo," amesema Kyando.

Amesema baada ya tukio hilo mlinzi huyo alikimbia kusikojulikana, na kuitelekeza silaha aliyokuwa nayo aina ya Shortgun, na Jeshi hilo linamtafuta na akikamatwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Aidha, amesema Jeshi hilo pia linawashikilia walinzi wenzake wanne, kwa ajili ya upelelezi zaidi juu ya tukio hilo, na kutoa wito kwa makampuni ya ulinzi kuacha matumizi holela ya silaha, sababu hilo ni tukio la pili kutokea mkoani Shinyanga ndani ya mwezi mmoja walinzi kusababisha mauaji.

Katika hatua nyingine Kamanda ametoa wito kwa wananchi ambao wanazunguka kwenye migodi ya madini, watii sheria na kuacha kuingia kwenye maeneo ambayo yanalindwa.

Post a Comment

0 Comments