Header Ads Widget

WAZAZI WAJENGE NJIA NA LUGHA SAHIHI ZA KUZUNGUMZA NA WATOTO KUHUSU AFYA YA UZAZI




Damian Masyenene, Mwanza

ILI kuhakikisha vijana walio katika rika balehe wanapata elimu sahihi ya afya ya uzazi  kwa wakati muafaka ambayo itawanusuru na mimba zisizotarajiwa, ngono zembe na hatari ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), wazazi wameshauriwa kutumia njia za kisasa, nyenzo na lugha sahihi ambazo zitafikisha ujumbe uliokusudiwa kuwasaidia watoto kufanya maamuzi sahihi ya maisha yao.

Ushauri huo umetolewa na Mshauri wa afya ya uzazi na malezi nchini, James Mlali katika mahojiano maalum na kipindi cha Mamamia kinachorushwa na East Africa Redio Aprili 6, mwaka huu huku akibainisha kuwa uoga, hofu na aibu kutoka kwa wazazi vimekuwa vikikwamisha jitihada za kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto wao.

Amesema wazazi walio wengi hawana maarifa ya kutoa elimu hiyo kwa watoto wao ambao wako kwenye rika balehe kwa sababu wao wenyewe hawakupewa elimu hiyo kutokana na kutoandaliwa hivyo hawajui watazungumza namna gani na watoto wao kuhusu mambo hayo ambapo wengi huyazungumza katika mafumbo.

Amezitaja njia rafiki na sahihi zaidi kufikisha elimu hiyo kwa watoto ni wazazi kujenga lugha inayoendana na umri husika, watalaam katika jamii waliofundishwa na kuelimishwa wakiwemo wataalam wa afya, maendeleo ya jamii na baadhi ya walimu, viongozi wa dini, wazazi wengine na ndugu wanaoaminika, vyombo vya habari na makambi ya watoto na vijana kuwafundisha watoto waweze kujitambua.

“Faida ya mzazi kuongea na watoto unawapa maarifa sahihi kwa wakati unaofaa na njia iliyo sahihi ambayo yatawapa ujasiri wa kufanya maamuzi sahihi kuliko wangeyapata kutoka kwa mtu wasiyemjua na huna uhakika atawapa maarifa gani, hii itakusaidia pia kujenga urafiki na uhusiano ambao utafanya wewe na mtoto wako muwe karibu na kuwawekea muongozo na msingi bora wa malezi,” ameshauri Mlali.

Akifafanua kwanini kumekuwa na ugumu kwa wazazi katika jamii nyingi nchini kuzungumzia masuala hayo na watoto wao alisema sababu kubwa ni mila na desturi ambazo zina miiko mingi, maarifa ya unyago na jando kutowekwa kwenye mitaala inayoeleweka ili upate elimu ya kutosha.

“Hii hofu na aibu inatokana na kutokuwa na maarifa pia miiko inasababisha hata kama anataka kuzungumza anaweza kuyakwepa au atayazungumza kwa mafumbo, matokeo yake mlengwa anayepaswa kupata maarifa ya kumuwezesha kufanya maamuzi sahihi anakosa na inabidi aanze kuokota okota anayoyasikia kwenye mitandao, kwa wenzake (makundi rika) au kwa wale ambao ni watu wabaya,” amesema Mlali.

Amesema japokuwa kuna jitihada nyingi za kufikisha elimu ya afya kwa vijana lakini bado nguvu haitoshi kwa sababu wazazi na watoto hawana muda wa kutosha, wazazi ambao hawajaandaliwa ni wengi zaidi na kuna upinzani kwa wazazi ambao wanaamini kuwapa elimu ya afya ya uzazi watoto ni kama kuwafungulia njia kwenda kujihusisha na vitendo vya ngono.

“Ukweli ni kwamba kwa kila jambo ikiwemo afya ya uzazi kuna mambo ambayo ni hasi na chanya kwahiyo watu wangepata ujuzi na maarifa wangeweza kuzingatia kutoa elimu ambayo itawafanya watoto wapate maarifa chanya inayomfanya ajenge picha au taswira ya maisha yake ya mbele na nini cha kufanya kuelekea kule,” amesema Mlali.

Jamila Hassan mkazi wa Mwanza ambaye ni mama wa watoto wawili anasema bado kuna ugumu wa wazazi kuzungumza na watoto kwa uwazi kuhusu masuala ya afya ya uzazi na badala yake wanatumia vitisho kuwakanya watoto jambo ambalo halisaidii sana ambapo anashauri wazazi kubadilika na kuendana na wakati kwa kufanya uamuzi sahihi ambao utawanusuru watoto wao.

Mwisho.


Post a Comment

0 Comments