Header Ads Widget

WANAWAKE WALIO KWENYE NDOA WASHAURIWA KUTUMIA NJIA ZA UZAZI WA MPANGO KUJENGA FAMILIA BORA, KUEPUKA MAAMBUKIZI YA VVU

Baadhi ya wanawake wakishiriki maandamano kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mkoa wa Mwanza ambayo hufanyika kila mwaka Machi 8.


Damian Masyenene, Mwanza

MBALI na kundi la vijana ambao wako kwenye hatari kubwa ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) na mimba zisizotarajiwa, kundi lingine ni wanawake na wanaume walio kwenye ndoa/kuishi pamoja ambao wameshauriwa kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango ikiwemo matumizi ya kondomu ili kupanga familia bora na kuepuka mimba zisitorajiwa na maambukizi ya VVU.

Inakadiriwa kuwa Tanzania kuna watu zaidi ya milioni moja wanaoishi na VVU huku matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya VVU/UKIMWI na Malaria Tanzania 2011-12 yakitaja kuwa kiwango cha maambukizi ni kikubwa zaidi miongoni mwa wanawake na wanaume ambao ni wajane na waliotalikiana pamoja na waliooana/kuishi panmoja (umri kati ya miaka 15-49).

Kwa mujibu wa Mwandishi wa kitabu cha ‘Sakramenti ya ndoa katika nyumba aminifu’ Paschal Maziku katika uzinduzi wa kitabu hicho mwaka 2017 mjini Shinyanga alisema wanandoa wamebainika kuwa vinara wa kupata maambukizi mapya ya VVU kutokana na kutozingatia sheria na kanuni za ndoa kwani wamekuwa wakioana kama fasheni na kujikuta baada ya miezi michache wakichokana na kufarakana ambapo kila mmoja huanza kuchepuka na kuleta maambukizi mapya ndani ya familia.
Mbunge Fatma Taufiq

Ili kuepuka maambukizi mapya ndani ya familia na kupanga wakati sahihi wa kupata watoto, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI, Dawa za Kulevya na magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Fatma Taufiq aliwataka wanawake kuwa na sauti ndani ya mahusiano yao ikiwemo kusisitiza matumizi ya kinga ili kupambana na maambukizi hayo.

Fatuma alitoa ujumbe huo jijini Mwanza Machi 8, mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya Mwanamke yaliyofanyika uwanja wa Nyamagana, alisema taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya inaonyesha waathirika wakubwa wa maambukizi ya VVU nchini ni wanawake huku chanzo kikitajwa kuwa ni baadhi yao kutozingatia matumizi ya kinga.

"Kama mwanamke utakuwa mwangalifu na mwaminifu na ukakataa ngono zembe inamaana kwamba Ukimwi utapungua ila usipotumia kinga hapo ndipo maambukizi ya ugonjwa huo yataenea,"

"Kuna baadhi ya wenzetu ambao wamekuwa wakifanya wakifanya biashara ambayo siyo nzuri kwa kutumia miili yao kujikimu na maisha, wanawake tukisema hapana tutasaidia kupunguza maambukizi ya Ukimwi nasisitiza wanawake wenzangu kataeni kutumika, huko kwenye mahusiano yenu ikibidi beba kondomu kwenye pochi mwenzako akiwa hana mwambie unayo usione aibu hayo ni maisha yako," alisema Tawfiq.

Aliongeza; " Kuna baadhi ya wanaume hawaendi kupima Ukimwi, wakipata matokeo ya wake zao wanaamini wako salama lakini inawezekana mwanaume akawa na maambukizi mwanamke akawa hana hivyo niwaombe muwahimize wakapime,"

Mmoja wa wanawake waliohudhuria maadhimisho hayo, Flora John alisema bado wanawake hawana sauti ndani ya mahusiano ya mapenzi kushawishi matumizi ya kondomu na njia za kisasa za uzazi wa mpango huku wakiogopa kushinikiza kwa kile kinachoelezwa kuwa wnahofia kuachwa, ambapo alishauri elimu iendelee kutolewa kwa makundi yote kutambua umuhimu wa uzazi wa mpango na kujikinga na VVU kwa wana ndoa.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike aliwataka wanawake ambao wenza wao hawajafanyiwa tohara kuwahamasisha kwenda kupatiwa matibabu hayo ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Ukimwi.

"Unapokuwa na mwanaume ambaye hajatahiriwa ni vyema ukamwambia akafanyiww tohara hii ni kwa usalama wake na wewe, pia watoto wenu wapelekeni kufanyiwa hivyo," alisema Samike.

TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807