Header Ads Widget

NGO SHINYANGA ZAONYWA KUFANYA KAZI KIMAZOEA KUPIGANIA HAKI ZA WANAWAKE NA WATOTO


Mkurugenzi wa Shirika la ICS Sokoine Kudely akizungumza kwenye kikao cha TAPO

Suzy Luhende, SHINYANGA

Mkurugenzi wa Shirika la Investing in Children and Their Society (ICS) mkoani Shinyanga Kudely Sokoine, ameyataka Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Shinyanga, yasifanye kazi kwa mazoea katika kupambania haki za wanawake na watoto, bali waendelee kujifunza kila siku ili kuweza kutokomeza ukatili unaofanyika katika jamii. 
Amebainisha hayo leo wakati akifungua rasmi kikao kazi cha TAPO la Shinyanga, ambacho kimeshirikisha  wadau wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto kilichoandaliwa na Shirika la GCI.

Sokoine amesema ili kuweza kuleta mabadiliko katika jamii na kuweza kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili, kila mmoja anatakiwa kujifunza kila siku jinsi ya kuwatetea wanawake na watoto ili waweze kupata haki zao.

"Hatutakiwi kufanya kazi kwa mazoea katika kupambania haki za wanawake na watoto, ili tulete mabadiliko tunatakiwa tuwe na ajenda ya pamoja, tujenge mahusiano na tuwe na mtandao wa pamoja, tuzingatie maadili ya kazi pia tunatakiwa tuwe na mkakati wa pamoja ili tuweze kuleta mabadiliko kwenye jamii yetu,"amesema Sokoine.

Mbarack Salum kutoka shirika la Rafiki SIDO amesema hali ya ukatili bado ipo japokuwa serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali mkoani hapa yanaendelea kupambana na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto lakini bado ukatili upo, mwaka jana binti mmoja wa kata ya Ilola alifanyiwa ukatili na wazazi wake wa kuoshwa dawa ya samba kisha kulazimishwa kuolewa.

" Msichana huyo alilazimishwa kuolewa na mwanaume ambaye alikuwa tayari kashapata maambukizi ya virusi vya ukimwi, hivyo kaishi nae mwaka mmoja kaachika baada ya dawa ya Samba kuisha nguvu kwa sababu wanasema dawa hizo zinaisha makali mwaka mmoja, kaachika na karudi nyumbani huku akiwa ameathirika na yeye kwa sababu alilazimishwa kuolewa bila hata kucheki afya yake na mwenzi wake, hivyo elimu iendelee kutolewa"alisema Salum.

Kwa upande wake mwakilishi wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (SPC) Suzy Butondo, amesema waandishi wa habari ambao kwenye mradi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto walikuwa na kazi ya kuelimisha jamii ili iondokane na ukatili, wamekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutopata ushirikiano kwa baadhi ya viongozi, na baadhi yao kutishiwa maisha kwa kuandika habari za ukatili.

Baadhi ya wawakilishi wa mashirika mkoani Shinyanga, wamesema wanaendelea kupambana na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, baadhi ya wananchi wameelewa lakini wengi bado wanaendekeza mila na desturi iliyojengeka, bado wanaendelea na ulawiti,mashuleni wanaozesha watoto wadogo kwa siri, wanawake wanapigwa na wanafunzi wanakatazwa kwenda shule kwa ajili ya kilimo.

Monica Masawe kutoka dawati la jinsia Y.W L amesema baadhi ya viongozi wa mitaa ushirikiano wao ni mdogo kwani wanakuwa na hofu kutokana na baadhi ya mambo yao hawataki kuingiliwa na wananchi, pia maeneo mengi ya migodi watoto hawaendi shule,wengi wanabakwa na kusababisha mimba za utotoni, pia wanaume wengi wanadai kufanyiwa ukatili lakini hawakipoti dawati la jinsia.

Aidha afisa maendeleo wa halmashauri ya Shinyanga Aisha Omary, amesema ili kuweza kutokomeza ukatili ni vizuri kufanya kazi kwa ushirikiano, na inapopatikana changamoto ni vizuri aliye kwenye tukio akatoa taarifa wakati akiwa eneo la kazi, ili aweze kupewa ushirikiano wa haraka na kuweza kutekeleza kazi yake kwa wakati.


Mkurugenzi wa Shirika la ICS Sokoine Kudely akizungumza kwenye kikao cha TAPO.

Washiriki wakipiga picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho.

Na Suzy Luhende, SHINYANGA.

Post a Comment

0 Comments