Header Ads Widget

SHIRIKA LA GCI LAUNDA MABARAZA YA WATOTO PUNI NA NYIDA WILAYANI SHINYANGA KUPAMBANA NA MATUKIO YA UKATILI

Meneja mradi wa Shirika la Green Community Inititives(GCI) George Nyanda akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa Kata ya Nyida na Puni wilayani Shinyanga kabla ya kuunda Mabaraza ya watoto.

Na Shaban Njia, SHINYANGA.

KATIKA kutokomeza vitendo vya kikatili kwa watoto na wanawake ngazi za vijiji na Kata, Shirika lisilo la kiserikali la Green Community Initiatives(GCI) limeunda mabaraza nane ya watoto katika kata za Puni na Nyida Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ili kutokomeza vitendo hivyo vinavyondelea ndani ya jamii.
 
Mabaraza hayo sita yameundwa katika ngazi ya vijiji na mawili ngazi ya Kata na lengo la uanzishwaji ni kuwawezesha watoto kutambua haki zao na namna ya kuzidai katika mamlaka husika hasa pale yanapotokea matendo ambayo yanawakamiza na kuwanyima uhuru.

Vijiji hivyo ni Puni, Buyubi, Nyida, Nduguti na Igebya huku kata zikiwa ni Puni na Nyida na ili yaweze kujisimamia na kujiendesha watoto hao watapewa mafunzo ambayo yatawafanya kutambua wapi wanatakiwa kupeleka mashauri ya ukatili wa kijinsia pale yanapotokea kwenye jamii zao.

Undwaji wa mabaraza hayo ni utekelezaji wa mradi wa mradi wa tuwalinde unaotekelezwa kata za Puni na Nyida Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa ufadhili wa Mfuko wa Wanawake Tanzania(WFT) na umeanza januari mwaka huu na unatarajia kufikia kikomo mwezi machi.

Meneja mradi wa Shirika la Green Community Inititives(GCI) George Nyanda aliyabainisha hayo jana wakati wa undaji wa mabaraza hayo alisema,mradi huo utawafikia na kuwapatia elimu ya ukatili wa kijinsia wananchi takribani 500 kati ya hao wazazi 200 wanafikiwa kwa njia ya vikundi vya malezi na makuzi na wanaume 300 watafikiwa kwa njia ya kuongeza ushiriki katika kupatana na vitendo hivyo

Alisema,Mabaraza hayo yatakuwa na washirikli 240 na yataongeza ushirikishwaji wa watoto katika hazi zao kwa kuzidai na kuzisema, kufanya maamuzi na kuripoti vitendo vya kikatili vinavyotendeka ndani ya jamii zao na kuhakikisha watoto wote kutoka vijiji vya kata za Puni na Nyida hawanyanyasiki na kufanyiwa vitendo viovu.

Naye Ofisa Maendeleo ya jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya ShinyangaEdmund Ardon alisema, mabaraza hayo yatasaidia kurahisha mawasiliano kwa watoto kwa sababu watoto wengi wanashindwa kutoa taarifa kwa watu wazima ila wao kwa wao ni rahisi kufikishiana ujumbe.

Alisema,mabaraza hayo yanaanzishwa kwa kila kijiji na kata kwa sababu ya uwepo mkubwa wa vitendo vya kikatili vilivyopo kwenye jamii na wanaoumia na vitendo hivyo ni watoto na akinamama nakwamba hata kama akinababa nao wanafanyiwa vitendo hivyo sio sawa na wanavyofanyiwa watoto na wanawake kwenye jamii.

“Kwenye jamii zetu tunazotoka kunafanyika vitendo vya kikatili lakini hayaripotiwi na wanaoumia ni watoto na wanawake,hivyo mabaraza haya yatakwenda kuwa suruhisho la kupunguza matendo haya na kuhakikisha wanafunzi wote hasa wa kike wanahitimu masomo yao katika hali ya usalama”Alisema Ardon.

Akizungumza kwa niaba ya Wenyeviti wa Mabaraza hayo, Mwenyekiti wa Baraza la watoto kijiji cha Nyida Doricus Yusufu alisema,atahakikisha wanawashawishi watoto wenzie kutoa taarifa za vitendo vya kikatili vinavyofanyika kwenye familia zao bila kuogopa hasa kwa kuzifikisha Ofisa ya Mtendaji wa kata au Ofisi ya Mwalimu Mkuu wao.

Alisema,watoto wengi katika kijiji chao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili kwa kunyimwa chakula wakati wanapotoka shuleni, kulazimishwa kwenda shambani kulima na kuchunga mifugo ya majirani zao kwa lengo la kupata kipato cha familia na anadai amekuwa akiyaona hayo.

“Hivi karibu mwanafunzi mwenzetu wa darasa la nne alibakwa wakati anatoka gulioni, wanamgambo walimkamata mtuhumiwa na kupelekwa Ofisni kwa mtendaji, hatujui kilichoendelea huko zaidi tulimuona mwanafunzi anarejea shuleni na sasa anaendelea na masomo, hivyo vitendo vya namna hii nitaviripoti”Alisisitiza Yusufu.

Meneja mradi wa Shirika la Green Community Inititives(GCI) George Nyanda akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kata ya Nyida na Puni kabla ya kuunda kwa mabaraza ya watoto.

Watoto wakiwa kwenye uundaji wa Mabaraza yao ambayo yatawasaidia katika mapambano ya kutokoza vitendo vya ukatili dhidi yao.

Na Shabani Njia, SHINYANGA.

Post a Comment

0 Comments