Header Ads Widget

WAZAZI NA WALEZI WASIKATE TAMAA YA KUSOMESHA WATOTO

 

Mwenyekiti wa mtaa wa Dome akionyesha fomu ambayo watajaza wanafunzi kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza.

Afisa elimu kata ya Ndembezi Akizungumza kwenye kikao cha mtaa wa Dome

Wazazi na walezi wa mtaa wa Dome kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuwasimamia na kufuatilia maendeleo ya mtoto shuleni, ili kuhakikisha wanafaulu vizuri na wanakuwa na maadili mema.

Hayo ameyasema mwenyekiti wa mtaa wa Dome Solomoni Najulwa kwenye kikao cha kuwatia moyo wazazi na walezi wasikate tamaa katika kuwaendeleza kielimu watoto waliofaulu kuingia kidato cha kwanza na kujua changamoto zilizopo.

Najulwa amesema katika mtaa wa Dome watoto wengi wanaofaulu ni wale watoto ambao wana mzazi mmoja wengine wanaishi na bibi zao, hivyo amewataka wasikate tamaa kuwasimamia na kufuatilia maendeleo yao shuleni hata Mara moja kwa wiki.

"Watoto Hawa wamefaulu kwenda kidato cha kwanza, nawaomba wazazi na walezi msichoke kuzungumza na watoto wenu, pia mshirikiane kwa karibu na walimu ili kujua maendeleo ya mtoto na kujua anafika kwa wakati shuleni na kurudi kwa wakati nyumbani"amesema Najulwa.

"Watoto wetu wengi wanaingia kwenye kurubuniwa na kuingia kwenye makundi mabaya kwa sababu hatuwafuatilii hatujui wanafika shule ama wanaishia njiani, hivyo ni vizuri tukawa karibu na watoto wetu ili wasijiingize kwenye makundi mabaya"amesema Najulwa.

Amesema watoto wanatakiwa kulelewa na wazazi watatu, mzazi, mwalimu na serikali, hao wote wakishikamana mtoto anakuwa na maadili mema na anafaulu vizuri masomo yake vizuri.

Kwa upande wake Afisa elimu kata ya Ndembezi Ustadius Mkulu amewataka wazazi wawanunulie watoto madaftari magumu yatakayodumu kwa muda mrefu ambayo watayatunza kwa miaka mnne, pia wawanunulie sare za shule zinazotakiwa ili waweze kwenda shule kwa wakati unaotakiwa.

"Lakini Kama ukikosa uwezo wa kununua sare za shule nenda nae shuleni ukaongee na mkuu wa shule, usikae na mtoto nyumbani kwa kukosa sare, pia elimu ni bure hakuna michango yeyote, kuna baadhi ya maneno watu wanapotosha wanasema ada imerudishwa ni uzushi tu si kweli hicho kitu hakipo, pelekeni watoto shule ni bule kabisa"amesema Mkulu.

Baadhi ya wazazi Joseph Mahalu akiongea kwa niaba ya wazazi amesema wanaahidi watakuwa bega kwa bega na watoto, pia watashirikiana na walimu kila Mara ili kuhakikisha watoto wao wanakuwa na maadili na wanafaulu vizuri.

Nao wanafunzi Recho Paul na Saimon Magembe wameahidi kuwa watakuwa na maadili mazuri hawatajiingiza kwenye makundi mabaya watahakikisha wafaulu vizuri na kuendelea katika masomo ya juu.

Baadhi ya wanafunzi waliofaulu kidato cha kwanza wakiahidi kusoma kwa bidii.



Attachments
Wazazi na wanafunzi wakimsikiliza mwenyekiti wa mtaa wa Dome Solomon Najulwa Akizungumza.
 
Suzy Luhende,Shinyanga

Post a Comment

0 Comments