Header Ads Widget

DAWATI LA JINSIA KUTOKA JESHI LA POLISI WATOA ELIMU YA UKATILI STENDI YA MABASI, WANAUME SHINYANGA WALALAMIKA KUNYIMWA UNYUMBA NA WAKE ZAO

Mkuu wa Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi wilayani Shinyanga Brightone Rutajama, akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika Stendi ya Mabasi wilayani humo.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

DAWATI la Jinsia Jeshi la Polisi wilayani Shinyanga, wametoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika Stendi ya Mabasi wilayani humo, huku baadhi ya wanaume wakilalamika kufanyiwa vitendo vya ukatili na wake zao kwa kunyimwa unyumba.

Elimu hiyo imetolewa leo, ikiwa ni maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia duniani, ambayo kilele chake ni Decemba 10 mwaka huu.

Akitoa elimu hiyo ya ukatili wa kijinsia Mkuu wa dawati hilo la Jeshi la Polisi wilayani Shinyanga Brightone Rutajama, amesema katika wiki hii ya maadhimisho ya kupinga vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia, jamii inapaswa kutafakali na kuchukua hatua ya kuachana na vitendo hivyo.

Amesema katika Stendi hiyo ya Mabasi kuna vitendo vingi vya ukatili ambavyo hufanyika, ikiwamo kutoleana lugha chafu za matusi ya nguoni, kupigana, ukatili wa kiuchumi, kisaikolojia, na hivyo kusababisha msongo wa mawazo na kufikia hatua ya watu kujinyonga.

“Wiki hii ni wiki ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, ambapo dawati la jinsia kutoka Jeshi la Polisi tumefika hapa Stendi ya Mabasi wilaya kutoa elimu hii, ili mkawe mabalozi wazuri wa kupinga vitendo vya ukatili ndani ya jamii,”alisema Rutajama.

Pia, amewataka wanaume wasisite kufika kwenye dawati hilo kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, ambavyo hufanyiwa na wake zao na siyo kukaa kimya, na hatimaye kujichukulia sheria mkononi na kusababisha madhara makubwa ikiwamo vifo.

“Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi hua tunapokea malalamiko ya watu wote bila ya ubaguzi, na kisha kuyatafutia ufumbuzi ikiwamo kutatua migogoro ya ndoa, lakini wanaotoa taarifa za kufanyiwa ukatili wengi hua ni wanawake na siyo wanaume, hivyo nawaomba na wanaume fikeni kwa wingi msione aibu,”aliongeza.

Naye Mratibu wa Polisi Jamii wilayani Shinyanga Magesa Marwa, akizungumza na Madereva wa Bajaji pamoja na Bodaboda kwenye Stendi hiyo, aliwataka kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Pia amewataka Madereva hao wa Bajaji na Bodaboda, katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, wazingatie sheria za usalama barabara, ili kutosababisha ajali ambazo ugharimu maisha ya watu na wengine kupata ulemavu.

Kwa upande wao wanaume ambao wamehudhulia kwenye elimu hiyo ya ukatili wa kijinsia kutoka dawati la Polisi, wamesema wanaume wengi kwa sasa wamekuwa wakifanyiwa vitendi vya ukatili wa kijinsia na wake zao kwa kunyimwa unyumba.

Walisema migogoro mingi sasa hivi ndani ya familia inasababishwa na wanawake kwa kuwanyima unyumba waume zao kwa kisingizio wamechoka na kazi, na hata kufikisha wiki mbili bila ya kukutana na mke wake, lakini wao wakiguswa tu kidogo wanakimbilia Polisi kushitaki.

"Tunashukuru kwa elimu hii ya ukatili wa kijinsia kutuletea hapa Stendi, lakini wanaume tuna nyanyasika sana siku hizi, wake zetu wanatunyima unyumba, lakini akijua unachepuka ndipo mgogoro unapoanzia na kufikia hatua ya kupigana," alisema Peter Makalanga.

"Waambieni na wake zetu wasitufanyie ukatili, lakini wao ukiwagusa tu tayari wanakimbilia Polisi kushitaki, hiyo siyo sawa, lakini ukiangalia chanzo cha yote hayo ni yeye mweyewe kuni nyima unyumba," aliongeza.

Aidha, alisema na migogoro inapotokea ndani ya familia, ndiyo chanzo cha kuachana na kusababisha watoto kukosa malezi bora, na hata kuwa machokolaa mitaani na wakike kujiuza.
Mkuu wa Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi wilayani Shinyanga Brightone Rutajama, akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika Stendi ya Mabasi wilayani humo.
Mratibu wa Polisi Jamii wilayani Shinyanga Magesa Marwa, akizungumza wakati wa utoaji elimu ya ukatili wa kijinsia katika Stendi ya Mabasi wilayani Shinyanga.

Katibu wa Stendi ya Mabasi wilayani Shinyanga Skerya Wilson akizungumza wakati wa upewaji wa elimu ya ukatili wa kijinsia kwenye Stendi hiyo.



Peter Makalanga akilalamika baadhi ya wanaume mkoani Shinyanga wamekuwa wakinyanyaswa na wake zao kwa kunyimwa unyumba lakini hawasemi.

Wafanyabiashara, Mawakala wa Mabasi, Boda boda na Bajaji, wakipatiwa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kutoka dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi.
Wafanyabiashara, Mawakala wa Mabasi, Boda boda na Bajaji, wakipatiwa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kutoka dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA.










Post a Comment

0 Comments