Header Ads Widget

RC MJEMA ACHARUKA WILAYANI KISHAPU, AFISA MANUNUZI AWEKWA PEMBENI, APIGA MARUFUKU KUPANDA BEI VIFAA VYA UJENZI


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akiwa kwenye ziara wilayani Kishapu.

Na Marco Maduhu, KISHAPU

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, ameendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya kimkakati wilayani Kishapu, pamoja na kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
 
Mjema amefanyaziara hiyo leo, kwa kukagua ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Sekondari Kishapu ,ukiwamo ujenzi wa vyumba vya Madarasa, Bweni, pamoja na matundu ya choo, huku akiwa ameambatana na Mkuu wa wilaya hiyo Joseph Mkunde, Mkurugenzi Emmanuel Johnson, wakuu wa Idara, viongozi wa Serikali na Chama.

Akizungumza na watumishi wa Halmashauri hiyo mara baada ya kumaliza kutembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Sekondari Kishapu, alisema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani humo.

Alisema katika Halmashauri hiyo kuna jumla ya ujenzi wa vyumba vya Madarasa 81, lakini kasi yake anaiona ndogo, na hivyo kuingiwa na wasiwasi wa kumaliza ujenzi huo kwa wakati.

“Halmashauri hii ya Kishapu mmeniangusha sana kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa, na nilipofuatilia nimeambiwa anaye kwamisha ni Afisa manunuzi, ambapo ili kununua vifaa vya ujenzi mpaka aamue yeye, hili limenikwaza sana,”alisema Mjema.

“Kuanzia sasa  Afisa Manunuzi wa Halmashauri hii (Zacharia Awe) apishe kwenye nafasi yake hadi pale ujenzi utakapoisha wa vyumba vya madarasa, na Mkurugenzi na kuomba unitafutie mtu mwingine ambaye ataziba nafasi yake na kuendana na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassani katika ujenzi wa vyumba vya Madarasa,”aliongeza.

Pia alitoa Maagizo kwa Mkuu wa usalama wilayani humo, Mkuu wa wilaya pamoja na Mkurugenzi, kusimamia Taratibu za kazi kwa Afisa Mipango, Ujenzi, Ardhi, pamoja na Fedha ili kuhakikisha wanafanya kazi kikamilifu katika ujenzi wa vyumba hivyo vya Madarasa.

Aidha, akizungumzia taarifa aliyopewa awali na Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi Maburugi Samweli, juu ya wafanyabiashara kupandisha bei ya vifaa vya ujenzi, amepiga Marufuku upandishaji wa bei hiyo, na kuagiza vifaa viuzwe kwa bei ya kawaida, ili kutokwamisha ujenzi huo wa vyumba vya Madarasa.

“Mheshimiwa Rais ameshatoa fedha za ujenzi wa madarasa mkoani kwetu, hivyo kama wafanyabiashara wakipandisha bei vifaa vya ujenzi, itabidi fedha ziongezwe na hilo sitakubali, na Taarifa nilizonazo huko viwandani bei haijapanda, hivyo sitaki mtu yoyote kutaka kukwamisha zoezi hili la ujenzi wa vyumba vya madarasa tutamchukulia hatua,” alisema Mjema.

Katika hatua nyingine Mhe. Mjema akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, aliwataka wawe na mshikamano, ushirikiano, pamoja na kujituma kufanya kazi, huku akiwataka wale wenye mapungufu wabadilike, na kama hawawezi ni bora wakapisha na kuachia watu wengine.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, alimwahidi Mkuu huyo wa Mkoa, kuwa Maelekezo yote ambayo ameyatoa atayafanyia kazi, ili kuhakikisha utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya Madarasa unafanikiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akizungumza na watumishi wa Halmashauri wilayani Kishapu.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, akizungumza kwenye kikao cha watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu.

Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakiwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa huo wa Shinyanga Sophia Mjema.

Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakiwa kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa huo wa Shinyanga Sophia Mjema.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akiwa kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa mindombinu katika Shule ya Sekondari Kishapu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akikagua ujenzi wa Bweni katika Shule ya Sekondari Kishapu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akiangalia ujenzi wa vyumba vya Madarasa katika Shule ya Sekondari Kishapu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akitoa maelekezo maboresho ya ujenzi wa ubao.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akiangalia maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya Madarasa katika Shule ya Sekondari Kishapu, Madarasa ambayo fedha zake zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassani, na kuonyesha kutoridhishwa na kasi yake.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, (kulia) akizungumza na Mfanyabiashara wa kuuza vifaa vya ujenzi wilayani Kishapu Mwenda Madaha, na kumuagiza marufuku kupandisha bei ya vifaa hivyo vya ujenzi, bali viuzwe kwa bei ya kawaida.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akiwa katika ziara yake wilayani Kishapu.

Na Marco Maduhu- KISHAPU.


Post a Comment

0 Comments