Header Ads Widget

MIMBA ZA UTOTONI KWA WANAFUNZI WA KIKE KISHAPU ZAWAIBUA MADIWANI, WADAU WATAKA HATUA ZICHUKULIWE

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo Novemba 11, mwaka huu. Picha na Suzy Butondo

Damian Masyenene
KUENDELEA kuripotiwa kwa matukio ya watoto wa kike ambao ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Kishapu kupatiwa mimba, madiwani wa hlamashauri hiyo na wadau wa haki za wanawake na watoto wameibuka na kutaka hatua zichukuliwe ikiwemo utoaji wa elimu ya afya ya uzazi.

Katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu cha Novemba 11, mwaka huu, Diwani wa Kata ya Seke Bugolo, Ferdinand Mpogomi alieleza kuwa katika shule ya sekondari iliyoko kijiji cha Mipa wanafunzi watatu walipimwa na kukutwa na ujauzito wakiwamo wanafunzi wawili wa kidato cha nne na mmoja kidato cha pili.

Mpogomi alisema jambo hilo ni la kusikitisha, aibu na lazima lisemwe hatua zichukuliwe ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinaichafua wilaya hiyo ambayo mara kadhaa imekuwa ikitajwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa mimba za utotoni nchini.

Diwani huyo aliungwa mkono na mwenzake wa kata ya Ngofila, Nestory Kalugula aliyesema changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu wa kilomita saba hadi 10 kwenda shule wakilazimika kuamka saa 10 alfajiri na kurudi nyumbani saa moja jioni wanajikuta kwenye vishawishi vinavysababisha mimba hizo na kukatisha masomo.

"Suala hili la watoto wa kike kuwa na ujauzito inatokana na shule kutokuwa na mabweni tunaiomba serikali itusaidie kutujengea mabweni ili kunusuru watoto wetu," alisema Kalugula.

Akitolea majibu ya hoja hizo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Emmanuel Johnson aliwaomba madiwani kupiga vita masuala ya mimba za utotoni kwani ni aibu kubwa kuonekana mwanafunzi akiwa na ujauzito na kushindwa kutimiza ndoto zao.

"Ni aibu kubwa kuona watoto wakiendelea kupata ujauzito na kukatisha masomo, sisi kama viongozi tunatakiwa tusimamie suala hili lisiendelee kutokea na hatutakiwi kujiingiza kwenye migogoro hiyo ambayo nasikia kuna baadhi ya viongozi wanahusishwa kwenye kuelewana ili mtuhumiwa wa mimba asikamatwe," alisema Johnson.

Kwa mujibu wa ripoti ya Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ya mwaka 2018 kulikuwa na kesi 105 za mimba za utotoni lakini nyingi zinazoripotiwa polisi hazifikishwi mahakamani ambapo kuanzia Januari hadi Septemba, 2019 jumla ya kesi 470 ziliripotiwa dawati la jinsia lakini ni 159 pekee zilifunguliwa mahakamani na 314 bado ziko chini ya uchunguzi wa polisi.

Pia mwaka 2018 kati ya kesi 473 za ukatili dhidi ya watoto zilizoripotiwa polisi, kesi 146 bado zinaendelea na uchunguzi, huku ripoti ya kitaifa ya ukatili dhidi ya watoto ilionyesha mkoa wa Shinyanga ukiwa juu kwa asilimia 59 za ndoa za utotoni.

Ripoti ya mkoa wa Shinyanga ya mwaka 2018/2019 wasichana 32 chini ya miaka 18 waliolewa na kunyimwa haki ya elimu ambapo katika watoto 3,451 walioacha masomo 1,116 walitokana na ukatili dhidi ya watoto.

Mdau wa haki za wanawake na watoto mkoani Shinyanga, Leah Josiah ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la Fikra Mpya alisema ulinzi wa mtoto ni jukumu la jamii nzima kuanzia kwenye familia hadi shuleni kwa walimu ili kuwaepusha na changamoto ya mimba hizo, huku akishauri kupewa kipaumbele elimu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike kuwaepusha na mimba, ndoa za utotoni na maambukizi ya VVU na magonjwa ya zinaa

“Suala la malezi ya mtoto linaanzia kwenye familia, mzazi au mlezi ni mtu wa kwanza kuhakikisha mtoto anakuwa anakuwa na maadili mema katika jamii kwahiyo lazima mtoto wa kike alindwe na aondolewe vikwazo kwa kuzingatia haki zake kwa vitendo ili atimize ndoto zao,” alisema Leah.

“Elimu ya afya ya uzazi ni muhimu itolewe kwa vijana wa kike ili waweze kujiepusha na mimba za utotoni, hili linaweza kufanyika kupitia majukwaa ya vijana balehe ili kuongelea changamoto zao ikiwemo matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa wanafunzi na kutafuta ufumbuzi wa namna ya kuzitatua changamoto hizo kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali za serikali,” alishauri.

Katika kikao cha asasi za kiraia na jeshi la polisi mkoani Shinyanga cha Novemba 5, mwaka huu baadhi ya wadau walilitupia lawama jeshi hilo kuwa sehemu ya kukwamisha mapambano ya ukatili kwa watoto kutokana na kasi ndogo ya ushughulikiaji kesi hizo na wakati mwingine kushriki kuzihujumu.

Mmoja wa wadau hao, John Myola ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la Agape Aids Control Program aliomba jeshi hilo kuwa na utaratibu wa kuwabadilisha vituo mara kwa mara maofisa wa dawati la jinsia kwani wanazigeuza kesi hizo fursa ya kiuchumi huku akieleza kwamba matukio hayo yanavunja moyo wadau wanaotetea watoto.

Alitolewa mfano kesi waliyoiripoti mtuhumiwa aliyekutwa na mwanafunzi wa darasa la tano (14) akiwa na ujauzito wa miezi mitano, alisema licha ya kukamatwa na vielelezo vyote lakini mtuhumiwa alipata dhamana na kutoroka huku akidai baadhi ya maofisa wa dawati hilo hutengeneza mazingira ya kupoteza ushahidi.

Inatajwa kuwa Tanzania ina asilimia kubwa ya mimba za wasichana wa shule, ambapo kwa mujibu wa Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya wa Tanzania wa mwaka 2015/16 asilimia 44 ya wanawake huwa wamezaa au wana mimba ya mtoto wao wa kwanza wakiwa na miaka 19.

Utafiti huo ulibainisha kuwa wasichana hawapati elimu ya kujamiiana na taarifa sahihi kuhusu dawa za kuzuia mimba, pia wanaupatikanaji mdogo wa huduma ya afya ya uzazi na hawana nguvu ya kujadili ngono salama na wanaume ambao kwa kawaida huwa wanawavutia na pesa, zawadi na ahadi za kuwasomesha au kuwaoa.


Post a Comment

0 Comments