Header Ads Widget

MAMA ADAIWA KUCHINJA WATOTO WAKE WAWILI KWA KISU SIMIYU, KISHA NA YEYE KUJIUA


Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi Blasius Chatanda

Na Costantine Mathias, Malunde 1 blog SIMIYU.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Mwanamke mmoja mkazi wa Lalago wilaya ya Maswa mkoani Simiyu amedaiwa kuwaua watoto wake wawili kwa kuwachinja na kisu, kisha na yeye kujiua.

Akizungumza leo Ijumaa Oktoba 22,2021 na waandishi wa Habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Blasius Chatanda amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mama huyo ambaye pia ni marehemu ndiye aliyetekeleza tukio la mauaji kwake na kwa watoto wake.

"Tarehe 22/10/2021 majira ya saa 8:30, kitongoji cha Mwatambuka, kata ya Lalago, Ng'washi Makigo (35) mkulima wa kijiji cha Gula ambaye ni mama wa watoto wawili Nseya Kisena (7) na Majaba Kisena (1.5) , watoto wadogo walikutwa ndani ya nyumba ya Luja Makigo wakiwa wameuawa kwa kuchinjwa", amesema Kamanda Chatanda.

Alifafanua kuwa uchunguzi ulionyesha alianza kumchinja mtoto wake mkubwa wa kike (Nseya) na kisha kumchinja mtoto wake mdogo wa kiume (Majaba) na hatimaye kujichinja yeye mwenyewe.

Alisema miili ya marehemu hao imekutwa yote ndani ya chumba kimoja nyumbani kwa Luja Makigo huku kisu kinachosadikika kutumika katika kutekeleza tukio hilo kikiwa kimebaki shingoni kwenye mwili wa mama huyo.

Mwenyeji wa Marehemu hao, Luja Makigo (mdogo wa marehemu) alibaini tukio hilo baada ya kurudi toka zahanati ya Gula alipokwenda kupata matibabu.

Kamanda Chatanda alitaja chanzo cha tukio hilo kuwa ni ugonjwa wa akili, kwani Luja ameeleza kuwa dada yake amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili kwa muda mrefu na alishawahi kufanya jaribio la kujiua kwa kujichana wembe shingoni miaka kadhaa iliyopita.

Aidha Kamanda Chatanda amewataka wananchi kuongeza umakini dhidi ya watu wanaosumbuliwa na wenye matatizo ya akili ili wasilete madhara katika jamii.Post a Comment

0 Comments